Mpanda FM
Mpanda FM
19 October 2026, 11:21 am

“fursa hii ya biashara ya hewa ukaa imeboresha miundombinu katika halmashauri yetu ya Tanganyika kwa kujenga vituo vya afya,vyumba ya madarasa kupata bima za afya tuendelee kuhifadhi mazingira“
Na.Bertod Chove
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamadi Masauni, amesema Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ina fursa ya kunufaika kiuchumi kupitia biashara ya hewa ukaa, sambamba na kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na kuongeza ajira kwa wananchi.
Akizungumza, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Katavi, amesema Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2050 imeweka msisitizo katika kuhakikisha biashara ya hewa ukaa inakuwa chachu ya uhifadhi wa mazingira, uzalishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha, amesema utaratibu wa mgawanyo wa mapato umeweka fursa muhimu kwa wananchi wanaomiliki maeneo yenye miradi ya hewa ukaa kunufaika na mapato yanayotokana na shughuli hizo, huku wakishiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira.
Hatua ambazo zinatoa fursa kwa wananchi wa Wilaya ya Tanganyika kuongeza manufaa ya kiuchumi kupitia uhifadhi endelevu wa mazingira, hivyo amewataka kutumia fursa hiyo kwa kuendeleza shughuli za uhifadhi na kushiriki katika miradi ya biashara ya hewa ukaa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Serikali.