Mpanda FM
Mpanda FM
4 June 2026, 11:30 am

“Tulikuta watoto hao wakiwa katika hali mbaya na mama wa watoto hao, baada ya muda mfupi aliishiwa nguvu tukawawahisha hospitali kwa ajili ya matibabu.”
Na Anna Milanzi -Katavi
Mama aliyefahamika kwa jina la Happiness Ngunda (25) pamoja na mtoto wake, Ibrahim, wamefariki dunia baada ya kuvuta hewa yenye sumu ya carbon monoxide iliyotokana na mkaa uliokuwa unawaka moto mghahawani katika mtaa wa Kampuni, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Tukio hilo limetokea wakati mama huyo akiwa katika mghahawa wake pamoja na watoto wake wawili, huku jiko la mkaa likiwa linawaka na mama na watoto wake wawili wakiwa wamelala ndani ya mghahawa huo.
Akizungumza baada ya tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa huo, Linus Felix, amesema mara baada ya kufika walikuta watoto hao wakiwa katika hali mbaya na mama wa watoto hao baada ya muda mfupi aliishiwa nguvu wakawakimbiza hospitali kwa ajili ya matibabu huku mume wa mama huyo akishangazwa kutokea kwa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Mpanda, Paul Swakala amesema, chanzo cha tukio hilo ni kuathiriwa na hewa yenye sumu ya mkaa iliyotokana na jiko lililokuwa likiwaka ndani ya mghahawa huo.
Dkt. Swakala amesema Gloria anaendelea kupatiwa matibabu, huku akitoa wito kwa wananchi kuepuka kuwasha majiko ya mkaa ndani ya nyumba au maeneo yasiyo na mzunguko mzuri wa hewa ili kuepuka madhara na vifo vinavyoweza kuzuilika.