Mpanda FM
Mpanda FM
18 June 2026, 4:36 pm

“familia ilimzika ndugu yao Joseph Kajumba Juni 12, 2026, lakini imeshtushwa na tukio la kukuta kaburi hilo limefukuliwa.”
Na John Benjamini -Katavi
Hofu na taharuki zimewakumba wananchi wa Kijiji cha Milala, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, kufuatia taarifa za kufukuliwa kwa kaburi la marehemu aliyezikwa hivi karibuni katika eneo hilo.
Taarifa za tukio hilo zimetolewa na mwenyekiti wa kijiji baada ya kupewa taarifa na baadhi ya wapita njia waliobaini hali isiyo ya kawaida katika eneo la makaburi.
Mmoja wa ndugu wa marehemu, George Kajumba, amesema familia ilimzika ndugu yao Joseph Kajumba Juni 12, 2026, lakini imeshtushwa na tukio la kukuta kaburi hilo limefukuliwa.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani, amesema Jeshi la Polisi limepokea taarifa hizo na tayari limeanza uchunguzi.
Kamanda Ngonyani ametoa wito kwa familia na wananchi wa Kijiji cha Milala kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, huku akionya dhidi ya vitendo vinavyohusishwa na imani za kishirikina ambavyo vinaweza kusababisha hofu na taharuki katika jamii.