Mpanda FM
Mpanda FM
4 May 2026, 6:21 pm

“Wanawake waombeeni waume zenu”
Na Anna Mhina
Wanaume wametakiwa kurejea katika maadili mema na kushirikiana na wenza katika kujenga familia imara yenye upendo, uwajibikaji, na mawasiliano mazuri ili kuweza kutengeneza familia bora.
Wito huo umetolewa na mchungaji kiongozi wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Living water lililopo mtaa wa Kwalakwacha manispaa ya Mpanda mkoani Katavi Rocky Petro kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanaume (CMF) na kuwataka kuacha tabia ya kutelekeza familia kwa kukimbia majukumu yao.
Kwa upande wao baadhi ya wanaume waliohudhuria maadhimisho hayo wameeleza sababu za kukimbia majukumu yao ni kutokujitambua na kushindwa kujishughulisha huku kaimu mwenyekiti wa idara ya wanaume kanisani hapo Reuben Kateba akiwasihi wanaume kusimamia majukumu yao kama baba.
Nao baadhi ya wanawake wamefunguka changamoto ambazo watazipitia endapo mwanaume atashindwa kuhudumia familia yake mbali na kuwaweka katika hatari ya vishawishi pia ukosefu wa elimu bora kwa watoto.
Maadhimisho hayo ya siku ya wanaume (CMF) yamefanyika mei 3 kwa Tanzania nzima ikiwa ni utaratibu wa makanisa ya TAG kila mwaka kuadhimisha sikukuu hiyo wiki la kwanza la mwezi mei.