Mpanda FM

RC Katavi asikitishwa viongozi wilaya ya Tanganyika kuchochea migogoro

21 November 2023, 5:59 pm

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko.Picha na Betrod Benjamini

Mrindoko amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Shaban J. Juma kufika ofisini kwake akiwa na nyaraka zinazoonesha ramani ya eneo la Luhafwe na mikataba yote ya uwekezaji waliyoingia na wawekezaji

Na John Benjamini-Katavi

Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesikitishwa na baadhi ya viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kujihusisha na uchochezi wa Migogoro katika eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji la Luhafwe lenye ukubwa wa hekta 46,000 (Ekari 115,000).

Mrindoko amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Shaban J. Juma kufika ofisini kwake akiwa na nyaraka zinazoonesha ramani ya eneo la Luhafwe na Mikataba yote ya uwekezaji waliyoingia na wawekezaji ikiwemo kiasi cha fedha Kilicholipwa halmashauri na hii ni Baada ya eneo moja kumilikishwa kwa wawekezaji zaidi ya mmoja.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi

Awali Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amemwambia RC Mrindoko kuwa katika eneo hilo, Halmashauri imepokea Fedha kutoka kwa kampuni mbili ambazo ni Seedland na Meru Agro kitendo ambacho kinaleta ugumu kwa eneo hilo kuendelezwa.

Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu .Picha na Anna Milanzi

Eneo la uwekezaji la Luhafwe lililotangazwa mwaka 2018 lina jumla ya Mashamba 116 ambapo kati ya hayo Mashamba 13 yana ukubwa wa Ekari 2000-5000, Mashamba 17 yana ukubwa Ekari 500, Mashamba 5 yana ukubwa wa kati ya Ekari 500-1000 na Mashamba mengine 81 yana ukubwa wa chini ya Ekari 500-1000.