Mpanda FM

Katavi,watuhumiwa 14 wafikishwa Mahakamani akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi halmashauri ya Mpimbwe

22 March 2024, 11:12 am

picha na Ben Gadau

watuhumiwa wote 14 wanashtakiwa na makosa 153 ikiwemo  utakatishaji wa fedha, kuunda genge la uhalifu na kugushi malipo kwa njia ya mtandao kinyume na utaratibu

Na Ben Gadau -Katavi

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imewafikisha  Mahakamani watuhumiwa 14 akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Catherine Mashala kwa kosa la ubadhilifu wa Fedha kiasi cha Shillingi Billioni 1 ,Milioni 232.

Baadhi ya watuhumiwa akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Catheline Mashala ( aliye mwanzoni katika picha) .Picha na Ben Gadau

Shauri namba 5 la Uhujumu Uchumi la Mwaka 2023 linalomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Catheline Mashala ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa na Watumishi wengine 13 wa Serikali Mkoani Katavi Watuhumiwa wote 14 wanashtakiwa kwa makosa 153 ikiwemo  utakatishaji wa Fedha, kuunda genge la uhalifu na kugushi malipo kwa njia ya mtandao kinyume na utaratibu.

Kesi hiyo imesomwa  katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Rebeka Mwalusako na upande wa Jamuhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Kelvin Bernard Mwaja .

Akizungumza nje ya Mahakama hiyo Mwendesha Mashtaka wa Serikali Kelvin Bernard Mwaja amesema katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi Washtakiwa wote wanashitakiwa kwa kosa la kuisababishia Serikali hasara

Sauti ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali Kelvin Bernard Mwaja akielezea kesi hiyo

Kwa upande wa Washtakiwa wameiomba Jamhuri kuharakisha upelelezi ili kesi hiyo ianze kusikilizwa baada ya kusalia Mahabusu kwa kipindi cha Miezi 8.

Kesi hiyo imeahirishwa Mpaka tarehe 28 Mwezi huu ambapo itasikilizwa tena katika Mahakama ya Hakimu  Mkazi Mkoa wa Katavi.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Stuart Kiondo ametoa wito kwa Watumishi wa Serikali kujiepusha na vitendo vya Rushwa pamoja na ubadhilifu wa Fedha za Serikali.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Katavi Stuart Kiondo .Picha na Ben Gadau