Mpanda FM

Marufuku kufyatua tofali Bonde Mto Misunkumilo

7 June 2023, 10:15 am

MPANDA.

Kufuatia katazo la kufanya shughuli za ufyatuaji tofali katika eneo la bonde la mto Misunkumilo mtaa wa Mpanda Hotel serikali ya kata imepiga marufuku shughuli hizo.

Akizungumza na Mpanda Radio Fm afisa mtendaji wa kata hiyo Carolina Medadi Yohana amesema kuwa baada ya katazo wamefanya mkutano wa hadhara na wananchi na kuwapiga marufuku kuendelea na shughuli za ufyatuaji wa matofali katika eneo la machinjioni na kueleza kuwa atakayekaidi katazo hilo hawatasita kumchukulia hatua za kisheria.

Mtendaji wa mtaa wa Mpanda Hotel Alfonce Maiko Nzyungu amesema kuwa serikali ya mtaa imepokea katazo hilo na kulifanyia kazi kwa kuhakikisha hakuna shughuli yoyote ya kibinadamu ambayo itafanywa ndani ya eneo la bonde la mto misunkumilo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mazingira kata ya Mpanda Hotel Emmanuel Mgina Machemba amesema kuwa kufuatia uharibifu mkubwa wa mazingira uliotokana na ufyatuaji wa matofali hadi sasa eneo hilo limebaki na mashimo ambayo ni hatarishi kwa maisha ya binadamu.

Barua ya mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Mpanda Sophia Kumburi iliyotolewa tarehe April 27, 2023, imeeleza juu ya kupiga marufuku kufanya shughuli za ufyatuaji tofali katika eneo la bonde la mto Misunkumilo.

#mpandaradiofm97.0

#katavists