Mpanda FM
Mpanda FM
30 April 2026, 2:06 pm

“Kijana aliyeokoka akikosa maadili ya kiroho anakosa uaminifu”
Na Anna Mhina
Uongozi wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) section ya Kabungu iliyopo kata ya Kabungu wilayani Tanganyika mkoani Katavi wamefanya kambi la maombi ya siku tatu kwa ajili ya kuombea maadili kwa vijana.
Akizungumza na Mpanda Radio FM wakati wa kufunga kambi hilo lililoamabatana na ziara ya viongozi wa jimbo, katibu msaidizi wa idara ya vijana jimbo la Katavi Magharibi Semeni Lusekelo ameeleza sababu za kufundisha somo la maadili kwa vijana ni kuwafanya wawe waaminifu hata wanapopata nafasi za uongozi serikalini.
Kwa upande wake mkurugenzi wa vijana section ya Kabungu mchungaji Lameck Garidi ameeleza lengo la kufanya kambi la maombi kwa vijana ni ili waweze kurejea katika misingi bora, kuwajengea hofu ya Mungu pamoja na kuishi maisha yenye maadili mema.
Nao baadhi ya vijana waliohudhuria kambi hilo la maombi wameahidi kuyaishi yale yote waliyofundisha na kutarajia maombi hayo yataleta mabadiliko makubwa kwao, katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kambi hilo la maombi ya siku tatu limefanyika katika kijiji cha Kamsenga kilichopo kata ya Kabungu wilaya ya Tanganyika na kuhudhuriwa na makanisa kumi likiwemo kanisa la Mchakamchaka, Majalila, Ifinsi, Bugwe, Kabatini, Kibo, Kamsenga, Silonge, Kasinde pamoja na kanisa la Kambanga.