Mpanda FM

Kampeni ya usafi yaanza kuleta matokeo Mpanda

6 November 2026, 2:54 pm

Bango lililowekwa katika eneo la stendi ya zamani la sheria za usafi. Picha na Restuta Nyondo

“tupo katika mpango wa kuongeza magari ili taka zinazozalishwa mtaani ziondolewe kwa wakati“

Na.Betord Chove

Kampeni ya usafi wa mazingira imeanza kuleta matokeo chanya, kufuatia kuimarika kwa hali ya usafi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa Oktoba 17, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph, ikiwa na lengo la kuongeza hamasa, kuimarisha ushiriki wa wananchi na kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hasan katika kuhakikisha shughuli za usafi wa mazingira zinazingatiwa ipaswavyo.

Akizungumza Novemba 4, 2026, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Bi. Sigilinda Mdemu, amesema uzinduzi wa kampeni hiyo ulioshirikisha wadau mbalimbali wa mazingira umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa na mwitikio wa wananchi katika kutekeleza shughuli za usafi wa mazingira.

Sauti ya Mkurugenzi

Aidha, Bi. Mdemu amewataka wananchi, wafanyabiashara na wadau wote wa mazingira kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika kujenga na kudumisha utamaduni wa usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa na madhara mengine yanayoweza kusababishwa na uchafuzi wa mazingira.