Mpanda FM
Mpanda FM
2 October 2026, 9:27 am

“kuweni mabalozi katika maeneo yenu katika kuchukua tahadhari“
Na. Ben Gadau
Shirika la Plan International kupitia mradi wa VUMA, limetoa mafunzo kwa makundi mbalimbali mkoani Katavi kuhusu namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, ikiwa ni pamoja na kutambua dalili, kuchukua tahadhari na kutoa elimu sahihi kwa jamii.
Akizungumza Afisa Afya wa Mkoa wa Katavi, Suzana Komba, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea washiriki uelewa kuhusu ugonjwa wa Ebola, ili waweze kufikisha taarifa sahihi kwa jamii na kuendelea kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, Afisa Afya wa Wilaya ya Tanganyika, Henric Sibale, ametaja baadhi ya dalili zinazoweza kuonekana kwa mtu mwenye Ebola kuwa ni pamoja na homa kali, uchovu wa mwili, maumivu ya viungo pamoja na kutokwa damu katika sehemu mbalimbali za mwili.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuwa mabalozi wa afya katika jamii, kwa kuitumia kutoa elimu sahihi kuhusu Ebola, namna ya kujikinga na umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Katavi Resort, Mpanda, yakihusisha makundi mbalimbali wakiwemo wazee maarufu, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waganga wa tiba asili pamoja na machifu, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii.