Mpanda FM
Mpanda FM
23 October 2026, 11:27 am

“hatuhitaji kusubiri mpaka mazingira ya vyanzo vya maji kuharibiwa ndio tutumie sheria“
Na. Betord Chove
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamadi Masauni, amelitaka Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) kufanya ukaguzi na uhakiki wa utekelezaji wa sheria ya mazingira nchini ndani ya kipindi cha wiki mbili ili kuhakikisha sheria hiyo inazingatiwa ipasavyo.
Masauni ametoa maelekezo hayo wakati akikagua shughuli za urejeshaji wa mazingira ya asili katika Mto Mkisi, Mkoani Katavi, eneo ambalo hapo awali liliathiriwa na shughuli za uchimbaji wa madini.
Aidha, ameitaka NEMC kutumia kipindi cha wiki mbili kufanya uhakiki wa kina ili kubaini kiwango cha uzingatiaji wa Sheria ya mazingira na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa maeneo yanayohitaji maboresho katika usimamizi wa mazingira.
Katika ziara hiyo, Masauni pia ametembelea mgodi wa Katavi Mining kwa lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini na kuhimiza uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za utunzaji wa mazingira ili kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.