Mpanda FM
Mpanda FM
10 November 2026, 7:39 pm

Na. Mwandishi wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limefanikiwa kuwakamata watu 15 waliojichukulia sheria mkononi kwa kufunga barabara kuu ya Mpanda – Sumbawanga huko katika eneo la kijiji cha Stalike, Kata ya Stalike, Wilaya ya Mpanda.
Tukio hilo limetokea Novemba 6, 2026 majira ya saa 9;30 usiku kwa watuhumiwa hao kuzuia magari kupita katika barabara hiyo kwa kuweka jeneza lenye mwili wa marehemu aitwaye Seni Kiberiti aliyefariki Novemba 5, 2026 baada ya kushambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili wake kutokana na kinachodaiwa ni mgogoro wa kugombea ardhi.
Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi lilifanikiwa kutuliza fujo hizo na kufungua barabara hiyo iliyokuwa imefungwa kwa kuondoa jeneza lililokuwa limewekwa katikati ya barabara na kufanikiwa kurejesha shughuli za usafiri kuendelea.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi liliendesha msako mkali na kuweza kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa 15 waliohusika katika tukio hilo la kufunga barabara.
Msako bado unaendelea wa kuwatafuta waliohusika katika tukio la kumshambulia Seni Kiberiti na kupelekea kifo chake.
Aidha, linatoa wito kwa baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi,na kufunga barabara kwani ni kinyume cha sheria, badala yake watumie njia sahihi kutatuwa migogoro pale inapojitokeza.