Jamii FM

Wadau wataka ushirikiano kuboresha vituo vya Day Care

30 September 2026, 08:25

Maafisa wa ustawi wa jamii na wadau wa vituo vya kulelea watoto Mchana (Daycare) wakifuatilia wasilisho la utekeleza wa programu ya PJT-MMMAM 2025/2026 katika ukumbi wa mikutano wa TCCIA mjini Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Wadau na wamiliki wa vituo vya Day Care mkoani Mtwara wameiomba Serikali kutumia lugha rafiki kwa waanzilishi wapya na kuwapatia ushauri ili kuboresha huduma za malezi na usalama wa watoto

Na Musa Mtepa

Wadau na baadhi ya wamiliki wa vituo vya malezi ya watoto mchana, maarufu kama Day Care, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kutoa mwongozo kwa waanzilishi wapya wa vituo hivyo, badala ya kuwaadhibu au kuvifungia vituo pale wanapokutana na changamoto.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha waanzilishi wa vituo hivyo kuboresha huduma na kutatua changamoto wanazokutana nazo katika maeneo yao.

Wadau hao wametoa ombi hilo Septemba 29, 2026, baada ya mkutano wa mapitio ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa mwaka 2025/2026, PJT-MMMAM, mkoani Mtwara, uliofanyika katika ukumbi wa TCCIA mjini Mtwara.

Wamesema baadhi ya waanzilishi wa vituo hivyo hawana uwezo mkubwa kifedha, bali wamekuwa wakianzisha vituo kwa kuguswa na changamoto zinazowakabili watoto katika jamii.

Kwa msingi huo, wamesema maafisa Ustawi wa Jamii wanapaswa kukaa na waanzilishi hao, kuwajenga na kuwashauri namna ya kuboresha vituo vyao ili vikidhi mahitaji na viwango vinavyotakiwa, badala ya kuchukua hatua za kuvifungia mara moja.

SAUTI YA WADAU NA WAMILIKI WA DAY CARE

Pamoja na kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya vituo kutokidhi vigezo vinavyotakiwa, Mwenyekiti wa vituo vya kulelea watoto mchana, Day Care, mkoa wa Mtwara, Selemani Mkonga, amesema kuna umuhimu wa jamii kuendelea kuanzisha vituo hivyo ili kuwahakikishia watoto mazingira salama wakati wazazi na walezi wakiwa katika harakati za kutafuta mahitaji ya msingi ya familia.

SAUTI YA SELEMANI MKONGA, MWENYEKITI WA DAY CARE MKOA WA MTWARA

Akielezea changamoto zinazowakabili waanzilishi wapya wa vituo vya Day Care, Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Mtwara, Bi. Teresia Ngonyani, amewataka wadau kuendelea kujitokeza kuanzisha vituo hivyo, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano pale changamoto zinapojitokeza.

Bi. Ngonyani amesema lengo ni kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki na wanalelewa katika mazingira salama na yanayozingatia mahitaji yao.

SAUTI YA BI. TERESIA NGONYANI, AFISA USTAWI WA JAMII MKOA WA MTWARA