Jamii FM
Jamii FM
22 October 2026, 06:33

NHIF yawataka wananchi mkoani Mtwara kujiunga na Bima ya Afya ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu, kuelekea uzinduzi wa dirisha la pili la usajili Oktoba 22, 2026
Na Musa Mtepa
Wananchi mkoani Mtwara wametakiwa kujiunga na Bima ya Afya ili kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Wito huo umetolewa Oktoba 21, 2026 na Meneja masoko na huduma kwa wateja wa mfuko wa Taifa wa bima ya Afya (NHIF), Anjela Mziray, wakati akitoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya, kuelekea uzinduzi wa dirisha la pili la usajili wa Bima ya Afya kwa wote unaotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 22, 2026 katika viwanja vya Sabasaba, Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Mziray amesema kuwa Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya na kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana hadi maeneo ya vijijini, hivyo wananchi wanapaswa kujiunga na Bima ya Afya ili kunufaika na huduma hizo bila kukabiliwa na gharama kubwa za matibabu.

Aidha, amesema kupitia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, Serikali imeweka vitita mbalimbali vya huduma za afya kwa gharama nafuu, ikiwemo kitita cha Faraja Afya kinachogharimu shilingi 150,000 kwa mwaka na kutoa fursa kwa kaya yenye watu wasiozidi sita kupata huduma za matibabu kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri, wilaya, mikoa hadi hospitali za taifa.

Akizungumzia uzinduzi wa dirisha la pili la usajili wa Bima ya Afya, Mziray amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Sabasaba, ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika, zikiwemo upimaji wa afya, usajili wa wanachama wapya wa Bima ya Afya, burudani ya muziki pamoja na huduma nyingine za afya.
Amesema mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
