Jamii FM
Jamii FM
30 September 2026, 21:25

Wananchi wa Naulongo wameiomba serikali ujenzi wa zahanati ukamilike kwa wakati ili waweze kupata huduma ya afya kwa ukaribu na kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo
Na Grace Hamisi
Mbunge wa jimbo la Mtwara mjini, Joel Nanauka, ameungana na wakazi wa mtaa wa Naulongo, kata ya Naliendele, manispaa ya Mtwara mikindani, katika zoezi la kuchimba msingi wa zahanati inayojengwa katika eneo hilo, Zoezi hilo limefanyika Septemba 29, 2026, na kushirikisha pia wakazi kutoka mitaa ya jirani.
Zahanati hiyo inalenga kusogeza huduma za afya karibu na jamii, ambayo kwa sasa hulazimika kusafiri takribani kilomita nne kufuata huduma katika maeneo ya Mbawala, Naliendele na Kituo cha Afya Ufukoni.
Akisoma taarifa ya utekelezaji, Mtendaji wa Kata ya Naliendele amesema hatua za awali zimeanza kwa kutumia shilingi milioni 50 kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri ya manispaa ya Mtwara mikindani.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mwalimu Hassan Nyange, amesema kituo hicho kitajengwa kwa viwango vya kisasa na kuwa mfano katika eneo hilo huku akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha huduma zote za msingi za afya zikipatikana Naulongo.
Aidha metoa wito kwa wakazi wa Naulongo kulinda vifaa vitakavyotumika wakati wa ujenzi, ili kuhakikisha kazi inaendelea bila vikwazo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mbunge Joel Nanauka amesema ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa mji, ambao wanahitaji kupata huduma muhimu za kijamii.

Naye Sofia Ally mkazi wa Naulongo kata ya Naliendele amesema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya afya, hasa wakati wa msimu wa masika.