Jamii FM

Wasio na ulemavu wanavyojinufaisha kupitia wenye ulemavu

24 April 2026, 14:27

Francis Chiwango Mkurugenzi wa shirika la MELODI. Picha na Msafiri Kipila

Tabia hiyo si tu inakiuka maadili ya kijamii, bali pia inawanyima watu wenye ulemavu heshima na haki zao za msingi. Kumtumia binadamu mwenzako kama chombo cha kujinufaisha ni kinyume cha sheria na haki za kibinadamu.

Na Msafiri Kipila

Katika siku za hivi karibuni, kumeripotiwa kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya baadhi ya watu wasio na ulemavu kuwatumia watu wenye ulemavu kama njia ya kujipatia kipato kwa manufaa yao binafsi.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Sharifu Kasimu amesema kuwa sababu kubwa inayochochea vitendo hivyo ni changamoto za kiuchumi, ambapo baadhi ya watu huwalazimisha watu wenye ulemavu kwenda kuomba ili kupata fedha. Amesisitiza kuwa hali hiyo si sahihi na inakiuka haki za watu wenye ulemavu.

Emannuel Majeshi Mwanasheria wa THRDC kitengo cha walemavu. Picha na THRDC

Kwa upande wake, mwanasheria na mtetezi wa haki za watu wenye ulemavu, Emmanueli Majeshi, amesema kuwa baadhi ya watu huwatumia watoto au watu wazima wenye ulemavu kuomba misaada, huku mara nyingi wakikosa kunufaika na fedha hizo. Ameeleza kuwa watu hao hutumika kama “chombo” cha kuamsha huruma kwa jamii, jambo ambalo ni unyonyaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Aidha, imeelezwa kuwa tabia hiyo si tu inakiuka maadili ya kijamii, bali pia inawanyima watu wenye ulemavu heshima na haki zao za msingi. Kumtumia binadamu mwenzako kama chombo cha kujinufaisha ni kinyume cha sheria na haki za kibinadamu.

Kutokana na hali hiyo, jamii imetakiwa kuchukua hatua madhubuti kukomesha vitendo hivyo. Serikali, mashirika ya kiraia pamoja na wananchi wanapaswa kushirikiana kulinda haki za watu wenye ulemavu. Vilevile, utoaji wa elimu kuhusu haki hizo utasaidia kubadilisha mitazamo ya jamii na kupunguza vitendo vya unyonyaji.

Bonyeza hapa kusikiliza Kipindi hiki