Jamii FM

Mwenyekiti awasaka wanafunzi majumbani

16 April 2021, 07:39 am

Mwenyekiti wa mtaa wa Geza ulole kata ya Majengo Manispaa ya Mtwara mikindani mkoani Mtwara Ndugu Jafari Likulangu Amekuwa na utaratibu wa kupita nyumba hadi nyumba kufuatilia mwenendo wa masomo kwa wanafunzi wa mtaa wake kwa kukagua daftari zao.

Mwenyekiti Wa mtaa wa Geza, Jafari Likulangu

Mwenyekiti huyo amekuwa akikagua daftari za wanafunzi wa Darasa la kwanza hadi kidato cha nne huku akiwa na lengo la kuwahimiza wanafunzi kuona umuhimu wa kusoma na hivyo itasaidia kupunguza utoro na kuongeza kiwango cha Vijana wasomi kwenye mtaa wake.

Isiyaka Salumu – mwanafunzi wa Darasa la saba shule ya msingi Tandika

Akiongea na Jamii fm radio Isiyaka Salumu mwanafunzi wa Darasa la saba shule ya msingi Tandika Mtwara amesema ni kweli Mwenyekiti huyo alifika nyumbani kwao na kukagua madaftari yake hali iliyompa faraja kwa kuwa hata siku moja wazazi wake hawakuwahi kukagua daftari za mwanafunzi huyo.

Yovina Mkapa mkazi wa Geza

Kwa upande wake Bi Yovina Mkapa mkazi wa muda mrefu wa Mtaa huo amesema hajawahi kuona Mwenyekiti kama huyo anayeweza kupita nyumba hadi nyumba kufuatilia mwenendo wa elimu wa wanafunzi na kuomba aendelee kufanya hivyo kwa kuwa atasaidia kupunguza utoro kwa watoto wao maana pale anapogundua mtoto haudhurii shuleni anawaita mzazi na mtoto Ofisini na kuzungumza nao kujua nini tatizo.