Jamii FM

“Wawezeshaji mmeaminiwa kafanyeni kazi” :- Mkurugenzi Mtwara Dc

28 February 2021, 10:46 am

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Bw. Maisha S. Mtipa tarehe 27 Februari, 2021 amewataka wawezeshaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia TASAF kuwajibika kwa walengwa huko vijijini kwakuwa serikali imewaamini.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara Bw. Maisha S. Mtipa akizungumza na wawezeshaji wa TASAF

Ameyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku sita kwa wawezeshaji 28 kutoka Mtwara Vijijini wanaoshughulika na miradi ya kipindi cha ari (PWP) yaliyofanyika ukumbi wa TTC kawaida Mtwara ambapo wanatarajiwa kuanza kufanya uibuaji katika jumla ya vijiji 57 vyenye utekelezaji wa mradi wa kaya maskini.

“…kuwepo kwenu si kwa upendeleo bali serikali na TASAF imewaamini na mmeonekana mnaweza kufanya shughuli hii muhimu ya kitaifa na sasa meiva….kwahiyo mkafanye kazi huku mkitambua sheria za utumishi wa umma zitatumika kwa wale watakaozembea…” ameeleza Bwana Mtipa.

Ameendelea kusema kuwa kupitia mada 22 walizofundishwa kwa kipindi chote cha siku sita ana imani kubwa kila mtu ameweza kuelewa na kuiva tayari kuanza kazi hiyo kwa ushirikiano, pia amewasisitizia kwa sasa wanatakiwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili muda wa uibuaji utakapofika iwe rahisi kwao kuwajibika.

Kwa mujibu wa Mratibu wa TASAF halmashauri ya Mtwara Bi. Zuena G. Myula, amesema wakati wa mafunzo hayo walitenga siku moja kwa wawezeshaji kwenda kufanya mafunzo ya vitendo katika kata ya Ziwani ili kupima ufanisi wa waliyofundishwa ambapo wengi wao wameonesha uelewa mkubwa.

wawezeshaji wa TASAF wakipatiwa mafunzo

Juu ya hapo imeelezwa kuwa miradi itakayoibuliwa itatekelezwa na walengwa wa kaya maskini ili waweze kujipatia kipato kupitia malipo ya ujira wa shughuli husika ambapo uibuaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu katika vijiji 57 vyenye mradi wa kunusuru kaya maskini.

Credit: Afisa Habari – Isaac Bilali