Jamii FM

Wananchi mikoa ya kusini kunufaika na mikopo ya kilimo

10 July 2023, 16:20 pm

Picha ya viongozi wa Bank ya TADB wakati wa uzinduzi. Picha na Musa Mtepa

Wananchi wa mikoa ya kusini Lindi, Mtwara na Ruvuma wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania  (TADB) Kanda ya Kusini  katika kupata uelewa na utaratibu wa kupata mikopo ili  kupata vifaa vya kisasa  vitakavyowezesha kuleta tija kwenye kilimo.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Benki hiyo Kanda ya Kusini Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kasim Majaliwa amesema kuwa wakulima hawana budi kwenda kupata mikopo  itakayowezesha katika shughuli mbalimbali za kilimo ili iweze kuleta tija.

Sauti ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mh. Kasim Majaliwa

Aidha Waziri Mkuu amewataka wanufaika wa mikopo kufanya matumizi sahihi ya fedha wanazokopeshwa ili kuendeleza miradi waliyoombea.

Sauti ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mh. Kasim Majaliwa

Akitoa salamu kwa Waziri mkuu , Mkuu wa Mkoa Mtwara Kanali Ahmed Abasi amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa umepokea zaidi shilingi bilioni  619.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati .

Sauti ya Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abasi

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini  Hassani Mtenga ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutoa huduma karibu na wananchi  huku akimwomba Waziri Mkuu kuangalia namna ya kutumia bandari ya Mtwara katika usafirishaji wa korosho.

Sauti za Mbunge Hassani Mtenga pamoja na Waziri na mbunge wa Newala Mkuchika

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwepo mkoani Mtwara hadi  Julai 14, 2023 katika ziara ya kikazi akikagua na kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika halmashauri zote zilizopo mkoani Mtwara ambapo hii leo atakuwepo halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.