Jamii FM

Mil.27.8 za Mapato ya ndani zatumika kutekeleza Afua za Lishe Mtwara Manispaa.

21 November 2022, 15:50 pm

Na Gregory Millanzi.

Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani imetumia shilingi milioni ishirini na saba na laki nane (27,800,000) kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za afua za lishe kwa Watoto wenye umri chini ya miaka mitano kati ya shilingi milioni ishirini na tisa (29,000,000) zilizotengwa katika bajeti ya 2021/2022 sawa na asilimia 92.

Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Lishe wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Emanuel Moshi kwenye kikao cha maandalizi ya mpango wa bajeti ya lishe ya mwaka 2023/2024 kilichofanyika Novemba 21,2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Afisa Lishe Moshi amesema kuwa, fedha hizo zitatumika kuhakikisha hali ya lishe kwa watoto chini ya umri wa Miaka 5 inaimarika na kuhakikisha Manispaa inakuwa kinara wa lishe kwa watoto Mkoani Mtwara.

Pia ametoa wito kwa watendaji wote kwa ngazi zote kuhakikisha wanatoa elimu ya Lishe kuanzia ngazi ya familia mpaka kata ili kuweza kupata Jamii yenye lishe bora.

Aidha kikao hiko pia kimepitisha mpango wa bajeti wa mwaka 2023/2024 ambapo Manispaa ya Mtwara-Mikindania imekisia kutumia shilingi milioni 71,700,000 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe ikiwemo kugharamikia matibabu ya Watoto wenye utapiamolo, ununuzi wa maziwa na virutubisho, kufanya ukaguzi wa mashamba ya chumvi Pamoja shughuli nyingine.

Kikao cha maandalizi ya bajeti kimehusisha wataalamu wa sekta mbalimbali kutoka halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara- Mikindani Pamoja na Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.