Jamii FM

Manispaa ya Mtwara yaanza kutoa chanjo ya Surua na Rubella

16 March 2023, 14:43 pm

Na Gregory Millanzi.

Kutokana na uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Surua na Rubella wataalamu wa afya kupitia kitengo cha afya kinga Manispaa ya Mtwara-Mikindani wameendelea kutoa huduma ya chanjo ya Surua na Rubella kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao hawajapata au kukamilisha chanjo hiyo.

Mtoa huduma ya afya kwenye kituo cha afya cha Likombe kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani akitoa huduma ya chanjo ya Surua na Rubela kwa mtoto. (Picha na Gregory Millanzi)

Zoezi hilo limeanza februari 20 na linatarajia kukamilika februari 27 mwaka huu, ambapo wahudumu wa afya wanapita nyumba kwa nyumba ili kuwabaini watoto ambao hawajapata chanjo na kuwapatia chanjo hiyo.

Manispaa ya Mtwara-Mikindani inatoa chanjo ya Surua na Rubella mara baada ya kubainika kwa uwepo wa vimelea vya ugonjwa huo kutoka kwa wagonjwa kumi na nne (14) wakiwemo wagonjwa sita wa Surua na wagonjwa nane wa Rubella.

Wataalamu wa Afya kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani wakitoa chanjo ya surua na Rubela kwa mtoto nyumbani, (Picjha na Gregory Millanzi)

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wamelipokea kwa zoezi hilo kwa umuhimu mkubwa kutokana na mlipuko huo kuanza katika baadhi ya maeneo.

“Asante sana Serikali kwa kuona namna yakuweza kutusaidia kwenye chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubella, maana kkwa mfano mimi nina mtoto wa miaka 3 lakini sikumbuki kama alipata chanjo, kwahiyo nimepokea vizuri zoezi hili maana mtoto anaweza kujikinga” alisema Halima Abdallah mkazi wa Majengo Mtwara.

kwa upande wake mratibu wa chanjo Manispaa ya Mtwara Mikindani Sylivera Rugaiganisa amesema zoezi linaenda vizuri na wananchi wameweza kujitokeza kwenye vituo na hata wanapotembelewa majumbani kupatiwa chanjo.

“Wazazi na walezi wamelipokea zoezi kwa hali ya juu sana na wameweza kushirikiana na watoa huduma wa Manispaa na kuwaleta watoto wao ili wapate chanjo na wanaendelea kujitokeza, pia nawahimiza kuwaleta watoto ili wapate chanjo hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5” Amesema mratibu wa chanjo Manispaa ya Mtwara Mikindani Sylivera Rugaiganisa.

Juma Rashid mkazi wa Naliendele manispaa ya Mtwara Mikindani ametoa wito kwa serikali kuhakikisha wanatoa huduma ya chanjo ya magonjwa ya milipuko mara kwa mara hasa kwa watoto ambao wanaishi pembezoni mwa Mjini maana wakati mwingine baadhi ya wazazi na walezi hawana elimu ya kutosha kuhusu magonjwa hayo, na wakati mwingine mtoto anapoumwa wanaanza kukimbilia kwa waganga wa kienyeji bila kujua tatizo ni la chanjo au wanapaswa kuwapeleka watoto hospitali.

“Napongeza Serikali kwa kazi kubwa mnayoifanya na nimesikia baadhi ya mazoezi ya chanjo hivi karibuni ila nashauri, kuwepo kwa mazoezi haya ya chanjo ya mara kwa mara hasa kwa sisi wananchi tunaokaa pembezoni mwa mji, maana kuna wakati mtoto anapatwa na maradhi ila kwakutokujua tunawahi kwa mganga wa kienyeji kwa kudhani ni mambo ya kishirikina, kuna tunapaswa kuwapeleka hospitali, ” amesema Juma Rashidi, mkazi wa Mtaa wa Sogea Naliendele.

Serikali imewaomba wananchi wote kuhakikisha wanawapeleka watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 kupata chanjo ya Surua na Rubella ili kuwalinda na magonjwa hayo. Chanjo inapatikana kwenye vituo vya afya na zahanati na pia inatolewa nyumba kwa nyumba.