Jamii FM

Watoto 41,339 kupata chanjo Mtwara

2 May 2021, 19:54 pm

Na Gregory Millanzi

Mkoa wa Mtwara unatarajia kuwapatia chanjo watoto 41,339 wenye umri wa kati ya mwezi 1 mpaka miezi 18 kwa mwaka 2021 ili kufikia lengo na kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya magonjwa yanayoepukika kwa chanjo.Akizungumza na Jamii FM Radio mratibu wa huduma za chanjo Mkoa wa Mtwara Serveus Kamala amesema, lengo ni kuwafikia wale wote wanaopaswa kupata chanjo na kwa kundi la watoto 41,339 wenye umri wa mwezi 1 mpaka miezi 18 kwa mwaka huu.Pia Kamala amesema zoezi la chanjo kwa watoto chini ya miaka miwili kwa mkoa wamefanikiwa kuvuka lengo la kitaifa la kuchanja kwa asilimia 95 kwa mwaka.

Picha kwa Hisani ya UN

“Lengo la kitaifa la uchajaji ni kuwafikia angalau asilimia 95 ya walengwa wote, sisi kama mkoa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika chanjo ya watoto wa chini ya miaka miwili kufikia lengo la kitaifa la kuvuka asilimia 95”. Amesema Kamala Serveus Kamala amesema kuwa, kwa sasa zoezi la chanjo limeboreshwa sana kuanzia ngazi ya mkoa mpaka kwenye wilaya ambapo kila kituo cha afya, zahanati na hospitali za wilaya huduma inapatikana na pia wengine wanafikiwa kwenye vijiji vyao na watoa huduma za afya kupitia huduma za mkoba.

“Uchanjaji umegawanyika katika makundi makubwa matatu, kuna wale ambao wanachanja kwenye vituo kutolea huduma, kuna ambao wanachanjwa kupitia huduma za mkoba (zaidi ya umbaki kati ya km 5 hadi 10) kutoka kituoni na wengine kupitia huduma tembezi ( zidi ya km 10 toka kituoni) ambapo hutembelewa kwenye vijiji vyao na watoa huduma za afya, hii yote ni kurahisisha upatikanaji wa huduma ya chanjo kwa walengwa wote ” amesema Kamala.

Kwa upande wake Hadija Rajabu mkazi wa Mtepwezi Manispaa ya Mtwara Mikindani amesema, yeye amenufaika sana na huduma ya chanjo na amepata kwa wakati tofauti na inavyosemwa kuwa inasumbua kupata.” Mimi nina mtoto na nimeshampatia chanjo tena wala haina usumbufu kupata tofauti na baadhi ya watu wanavyodai kuwa ukienda kwenye kituo cha afya unasumbuliwa kupata chanjo, sio kweli na nawashauri wazazi na walezi wawapeleke watoto wakapate chanjo kwa ajili ya afya yao ya sasa na ya baadae.

“Kila ifikapo tarehe 24 mpaka 30 Aprili kila mwaka ni siku ya maadhimisho ya wiki ya chanjo kitaifa, ambapo kwa mkoa wa Mtwara inatarajia kuwafikia walengwa wa chanjo 1,507,426 kwa mwaka 2021 ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa surua endapo jamii haitakuwa imepata chanjo kikamilifu na kwa usahihi.

Na Gregory Millanzi