Akitoa maelezo juu ya chanjo
Jamii FM

Masasi yazindua kampeni ya chanjo ya Polio kwa Watoto

30 April 2022, 06:42 am

Na Gregory Millanzi.

WILAYA ya Masasi mkoani Mtwara imezindua rasmi Kampeni ya utoaji wa chanjo ya matone ya ugonjwa wa Polio kwa watoto zaidi ya 55,234 walio chini ya miaka mitano lengo likiwa ni kuwakinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Akizungumza katika Uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Polio kwa watoto

Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 27.04.0222 mjini Masasi ambapo mgeni rasmi katika kikao cha uzinduzi huo alikuwa ni mkuu wa wilaya ya Masasi, Claudia Kitta ambaye aliwakilishwa na katibu tawala wa wilaya hiyo , Mohamedi Azizi.

Watu waliohudhuria Uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Polio kwa watoto

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye Uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Polio kwa watoto

Akizungumza na wajumbe wa kikao, hicho Mratibu wa chanjo Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Blandina Mpunga amesema kuwa zoezi la kampeni hiyo ya Polio itafanyika nyumba kwa nyumba na itafanyika kwa siku nne kuanzia mapema mwezi ujao.

Amesema kuwa jamii wilayani Masasi inapaswa kujitokeza kwa wingi na kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo na kuweza kuwafikia watoto wote ambao ni walengwa.

Amesema kwa Halmashauri ya wilaya ya Masasi watoto ambao wanatarajia kuchanjwa katika kampeni hiyo ni 41,438 na upande wa Halmashauri ya mji Masasi, 13,796

Akitoa maelezo juu ya chanjo

Awali akifungua kikao hicho, katibu tawala wilaya ya Masasi, Mohamedi Azizi ametoa wito kwa wanamasasi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwataka waendesha kampeni hiyo kuhamasisha jamii ili kila mwananchi aweze kufahamu zoezi hilo la kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa Polio.