Jamii FM

TRA Mtwara yavuka malengo makusanyo Julai-September 2022

24 November 2022, 15:00 pm

Na Gregory Millanzi.

MAMLAKA ya Mapato Nchini (TRA ) Mkoa wa Mtwara imevuka lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 8.902 kati ya Julai na Septemba 2022 ikiwa sawa na asilimia 110 .67 ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 8.043 kwa Kipindi hicho, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mamlaka wanatarajia kukusanya shilingi Bilioni 56.049.

Meneja wa TRA Mkoa wa Mtwara Naomi Mwaipora
ameeleza kuwa biashara ya usafirishaji wa Korosho kupitia Bandari ya Mtwara na biashara ya mpakani mwa Nchi Jirani ya Msumbiji ingeongeza mapato zaidi.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Mamlaka hiyo ilifanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 55.464 sawa asilimia 173 ya
lengo la
makusanyo ya Shilingi Bilioni 32.068.

Akizungumzia leo katika maadhimisho ya siku ya shukrani ya mlipa kodi yaliyofanyika Mkoani hapa Meneja huyo wa TRA amesema, mafanikio hayo makubwa ya makusanyo ya kodi ni matokeo ya walipa kodi wazalendo, waliohamasika na wenye kujitoa kwa dhati.

Licha ya kuwa na mafanikio hayo lakini kumekuwa na baadhi ya changamoto ikiwemo suala la utunzaji wa kumbukumbu za biashara kwa baadhi ya Wafanyabiashara, elimu ya mlipa kodi, matumizi ya mashine za kieletroniki.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Idara ya Upelelezi na Kodi Felisiana Nkane Kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA Nchini amesema, Mamlaka hiyo inaendelea kutekekeza mikakati inayoweza kuboresha namna ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kutoa huduma bora kwa mlipa kodi hivyo wako tayari kupokea maoni na mapendekezo yanayoweza kuleta tija zaidi katika kazi zao.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Kanali Patrick Sawala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameipongeza Mamlaka hiyo kwa mafanikio makubwa ambayo yametokana na utendaji wao mahiri na makini, kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, mipango mizuri ya kazi.

“Kama mnavyofahamu Mamlaka ya Mapato Tanzania ni chombo cha Serikali ambacho kina jukumu la kuratibu na kukusanya mapato ya Serikali Kuu kwa mujibu wa Sheria za kodi”,Amesema Sawala

Katika maadhimisho Mamlaka hiyo imetoa vyeti na vikombe kwa walipa kodi kama ishara ya shukrani ili kuleta hamasa kwa walipa kodi wengine waweze kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Nchi yao.

Mwisho.