Jamii FM

Msitegemee Korosho tu: Makamu rais TCCIA

9 March 2021, 09:35 am

Wakulima mkoani Mtwara wameshauriwa kulima kilimo bora na cha kisasa ili kuendana na fursa mbalimbali za masoko na mazao ya kibiashara ikiwemo zao la muhogo.

Akitoa wito huo jana Machi 08,2021 kupitia Jamii FM Radio Makamu wa rais wa chama cha wafanyabiasha, viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoani Mtwara Swallah Said Swallah amesema kuwa Wakulima wanapaswa kuongeza thamani ya zao hilo ili wanufaike kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Makamu wa rais wa chama cha wafanyabiasha, viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoani Mtwara Swallah Said Swallah

Ameeleza kuwa Miaka ya hivi karibuni Serikali ya Jamhuri ya watu wa China imeingia mkataba na Serikali ya Tanzania ikihitaji takribani tani Milioni mbili za Muhogo kwa mwaka, jambo ambalo wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuandaa zao hilo kwa ubora wa hali ya juu.

Hata hivyo Swallah Said Swallah amesisitiza Wakulima wa Mtwara kutotegemea zao la korosho pekee kama kilimo cha biashara, bali wanapaswa kulima kulingana na fursa zilizopo na kuwataka wajishughulishe na mazao mengine kama Ufuta, Mbaazi, karanga, Muhogo na mazao mengineyo.