Jamii FM

Kujihusisha na kilimo cha Bangi, kifungo cha miaka 30 jela

30 November 2022, 13:12 pm

Na Gregory Millanzi.

Afisa sheria Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za Kulevya nchini, Christina Rweshabura amesema kuwa ukibainika kujihusisha na kilimo cha bangi na Mirungi , sheria inatoa kifungo cha miaka 30 jela.

Rweshabura amesema kuwa, Mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini yanaongozwa na sheria ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya , sheria hiyo inaharamisha mambo mbalimbali yakiwemo ; Kilimo cha bangi, Mirungi, Kumiliki mbegu zinazozalisha dawa za kulevya, inaharamisha usafirishaji wa dawa za kulevya, kujihusisha kwa namna yoyote kinyume cha sheria na kemikali bashirifu, kumiliki mashine,vifaa na maabara kwa lengo la kutengeneza dawa za kulevya.

Christina Rweshabura amesema kuwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya imeazimia kupambana vilivyo na wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuhakikisha tatizo la dawa hizi linakuwa historia Nchini.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Kinga na Huduma za Jamii kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Moza Makumbuli amewaomba wananchi kutojihusisha na kilimo au biashara ya Bangi na Mirungi maana sheria iko wazi na ukikutwa na hatia ni jela miaka 30.

Pia amewaasa Wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa kwa vyombo vya dola hasa kwa wanaouza na kutumia Madawa ya kulevya ili kuhakikisha mtandao huo unathibitiwa na kutokomezwa kabisa.

Amezungumza hayo Novemba 29, 2022 kwenye maonyesho ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambapo kitaifa yanafanyika kwenye viwanja vya Ilulu Mkoani Lindi, kilele cha maandhimisho hayo ni tarehe 01 Desemba 2022 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani.