Jamii FM

Mtu mmoja afariki na wengine 11 majeruhi kwenye ajali kiwandani Dangote

8 July 2021, 16:17 pm

Na Gregory Millanzi,

MTU mmoja amefariki Dunia, watatu hali zao siyo nzuri na wengine nane kujeruhiwa kufuatia ajali iliyookea kwenye Kiwanda cha kuzalisha Saruji (DANGOTE ) kilichopo Kijiji cha Hiyari halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Tukio hilo limetokea Julai 7 mwaka huu majira ya saa 9:30 Alasiri ambapo udongo uliopo kwenye kinu cha kuzalisha Saruji kudondoka na kusababisha vumbi hali iliyopelekea watu hao kupata taharuki na kati yao mtu mmoja kuvua mkanda na kudondoka chini kisha kufariki wengine kupata majeraha ya moto yanayotokana na sehemu ya kinu.

Akitoa taarifa kuhusu kutokea kwa tukio hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya aliyeongozana na waandishi wa Habari, Meneja uzalishaji wa kiwandani hapo Subash Samantaray amesema kuwa Julai 5 mwaka huu walisimamisha shughuli za uzalishaji majira ya saa 12 jioni kwa ajili ya kufanya ukarabati katika kinu hicho ili kuondoa udongo ambao umeganda ndani ya kinu kinachotumika kutengeneza Saruji kiwandani hapo.

“Tulianza kuondoa maudongo udongo yale yalioganda ganda kwenye kinu husika ambacho kinatumika kutengeneza joto kwa ajili ya kutengeneza Saruji kwa muda kama wa siku tatu hivi kwahiyo wakati mchakato unataka kuanza tulitoa taarifa katika maeneo yote yale ambayo nguvu kazi itakuwa ikifanyika kwahiyo wale watu waliokuwa wakifanya Kazi kwenye lile bomba la linalopitisha mvuke kutoka kwenye chanzo kabisa cha kutengeneza joto kulitokea tukio la kudondoka dongo kubwa sana ambalo lilikuwa limeganda na kushuka chini na kutengeneza vumbi vumbi fulani likaanza kutawanyika kuelekea kwenye lile eneo ambalo watu walikuwa wamekaa”,

“Baada ya lile vumbi watu wakawa wanakimbia sasa mtu moja akafungua ule mkanda akadondoka kwahiyo jumla kulikuwa na watu 12 ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye lile eneo walikuja kuunguzwa na huo mvuke ulivyokuwa kwenye hilo vumbi vumbi baada kudondoka huo udongo wakapata hapa huduma ya kwanza badae wakapelekwa Ligula Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya matibabu kwahiyo yule mmoja ambaye alifungua mkanda alifariki baada ya kudondoka chini aliumia sehemu ya kichwa na wale wengine ambao walijeruhuwa wanaendelea vizuri”,amesema Samantaray

Mkurugenzi wa kiwanda hicho cha Dangote Appavoo Annadurai alisema kuwa shughuli hizo ambazo zikiendelea kiwandani hapo ni shughuli za kawaida kwani zimekuwa zikifanyika katika kiwanda hicho ikiwemo kukarabati na kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa lakini ilipotokea kudondoka kwa udongo huo ambao ni zaidi ya mita 100 kwenda ndani na kutengeneza vumbi hilo kwani hawakutarajia kwa hicho kilichotokea.

Mshauri rasirimali mali watu kiwandani hapo Bala Zango amewaomba wadau au jamii kwa ujumla kwamba pale panapotokea tukio ni vema kupata uthibitisho, taarifa sahihi juu ya tukio husika kuliko kutoa taarifa zenye upotoshaji hasa kufuatia taarifa za zinazotolewa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo kuwa ni ajali iliyotokana na mripuko wa Gesi kimsingi amekanusha kuwa taarifa hiyo siyo sahihi kwa kuwa haijathitishwa nakuahidi kiwandani hapo kuendelea na shughuli zake za uzalishaji kama kawaida.