Jamii FM

Mkuchika Awataka wazazi kuchangamkia fursa ya elimu

4 December 2021, 23:15 pm

“Hali ya Elimu kwa Wilaya ya Newala hasa kwa Kidato cha sita tumekuwa Tukifanya vizuri kwa muda sasa, kwa matokeo ya Kidato cha sita Shule ya Kiuta ambayo ina Wasichana pekee yake kwa kidato cha tano na sita na shule ya Wasichana Nangwanda ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye matokeo ya Mitihani ya Mwisho kimkoa, Hii inaonyesha hali ya Elimu kwa Wasichana Newala imehamasika sana”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum Kapten Mstaafu George Mkuchika

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum Kapteni Mshaafu George Mkuchika akiwa kwenye ziara ya kukagua Miradi ya Ujenzi wa Madarasa ambayo imepatiwa fedha na Serikali kupitia Mpango wa Uviko

Na Gregory Millanzi, Mtwara

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum Kapten Mstaafu George Mkuchika amewataka wazazi na walezi mkoani Mtwara kuchangamkia fursa za kielimu kwa kuwaendeleza watoto wao wanaochaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza na tano kwa kuwa serikali imewekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya shule nchini.

Waziri Mkuchika alisema hayo kwa nyakati tofauti jana wakati akizungumza kwenye mikutano ya hadhara na wakazi wa vijiji vya Nanguruwe, Tawala na Mkunya kata ya Mkunya wilaya ya Newala na kuwasisitiza kuwa elimu ndio msingi wa kuondoa umaskini katika kaya.

moja ya madarasa yanayojengwa

Amesema Serikali imewekeza kwenye ujenzi wa shule ili kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule na kupata haki ya elimu.

“Kwa Wilaya ya Newala kwa sasa Hakuna Mtoto yeyote anayemaliza Darasa la Saba na kufaulu anakaa nyumbani, watoto wote wananafasi ya kuanza kidato cha kwanza na kuendelea na masomo ya sekondari kwasababu Serikali imejenga miundombinu ya shule, hivyo wazazi na walezi mnatakiwa kuwapeleka shule watoto kwa maendeleo ya kaya na Taifa kwa ujumla” Alisema Mkuchika.

Waziri Mkuchika alisema mbali ya ujenzi wa madarasa kupitia fedha za Uviko 19 zilizotolewa na wahisani , Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kutoa fedha shilingi Milioni Mia Tano kwa kila jimbo kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ambayo inatakiwa kukamilika kwa wakati ili kuendelea kuondoa adha kwa watoto kutembea umbali mrefu.

Waziri George Mkuchika ambae pia ni Mbunge wa Newala Mjini, alisema kwa sasa Hali ya Elimu hasa kwa upande wa kidato cha tano na sita imekuwa kubwa sana kwa Wilaya ya Newala, ambapo kwa Matokeo ya Kitaifa ya Mtihani wa kidato cha sita Shule ya Kiuta imekuwa ya kwanza kimkoa.

“Hali ya Elimu kwa Wilaya ya Newala hasa kwa Kidato cha sita tumekuwa Tukifanya vizuri kwa muda sasa, kwa matokeo ya Kidato cha sita Shule ya Kiuta ambayo ina Wasichana pekee yake kwa kidato cha tano na sita na shule ya Wasichana Nangwanda ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye matokeo ya Mitihani ya Mwisho kimkoa, Hii inaonyesha hali ya Elimu kwa Wasichana Newala imehamasika sana” Amesema Mkuchika.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum Kapten Mstaafu George Mkuchika ambae Pia ni Mbunge wa Newala Mjini anaendelea na Ziara ya Kikazi katika Jimbo lake kwa ajili ya Kuwashukuru Wapiga Kura wake, ambapo hakuja kuwashukuru kwa sababu baada ya uchaguzi alikuwa nje ya nchi kwa ajili ya Matibabu na alivyorudi kulikuwa na katazo la Mikusanyiko ya ugonjwa wa Uviko 19.