Jamii FM

NMB yasaidia Vifaa vya kujifungulia mama wajawazito Likombe Mtwara

27 May 2022, 14:44 pm

Meneja wa NMB Kanda ya kusini Bi Janeth Sango akimkabidhi vifaa ya kujifungulia mama wajawazito Afisa Tarafa wa Mtwara Mjini ambae alimwalilisha Mkuu wa Wilaya Mh Said Kayangu kwenye kituo Cha Afya Cha Likombe Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Na Gregory Millanzi

Katika Kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha Sekta ya afya hapa nchini, Benki ya NMB Kanda ya Kusini imekabidhi viti mwendo vitano (Wheel Chair) na Vitanda Viwili vya kujifungulia (Delivery beds) kwa akina mama wajawazito vyenye thamani ya shilingi Milioni Tano(5,000,000) Katika Kituo Cha afya Likombe kilichopo Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Akizungumza mara baada ya kupokea Vifaa hivyo Mei 23,2022 Afisa Tarafa ya Mtwara Mjini ambae pia alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mtwara ndugu Said Kayangu ameipongeza benki hiyo Kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika kuleta Maendeleo.

“Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inatambua mchango wa NMB , inatambua namna Benki inavyoshiriki kikamilifu kwa Serikali, na namna inavyomuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katika kuleta Maendeleo”amesema Kayangu.

Aidha Kayangu amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara -Mikindani na pamoja na baraza la Madiwani kwa kuona umuhimu wa kusukuma Maendeleo mbele na kutekeleza miradi inayoboresha Sekta ya afya.

Nae Mkurugenzi wa Manispaa hii Col Emanuel Mwaigobeko ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada walioutoa Kwani imeipunguzia mzigo Manispaa Kwa kuwa fedha ambazo zingetumika kununua Vifaa hivyo itasaidia kutekeleza miradi mingine ya Maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini Bi.Janeth Shango amesema kuwa Benki hiyo inatambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita na kwamba Wana wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha inatumia faida wanayoipata kutoa msaada kwa jamii hasa Katika Sekta ya afya na Elimu.

Vitanda vya kujifungulia mama wajawazito ambavyo vimetolewa msaada na Banki ya NMB Mtwara

Amesema kuwa Benki hiyo imejiwekea utaratibu wa kuendelea kutoa misaada kwa Jamii na Kwa mwaka huu imetenga shilingi bilioni Mbili (2,000,000,000) kusaidia Katika Sekta hizo.

Bi. Agness Kalanje mkazi wa Matopeni ameishukuru Benki ya NMB kwa Msaada walioutoa Kwani itasaidia kupunguza foleni kwenye Utoaji wa huduma kwa akina mama wanaojifungua na hospitali itaweza kuhudumia idadi kubwa ya akina mama hao kwa wakati mmoja.