Jamii FM

Waziri Mkuu Majaliwa kuwasha mwenge wa Uhuru Mkoani Mtwara

30 March 2023, 18:29 pm

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Majaliwa Kasim Majaliwa. Picha na Bunge la Tanzania

Mwenge wa Uhuru wa Tanzania unatarajiwa kuwashwa Mkoani Mtwara Ili kuanza kuzunguka Tanzania nzima kwaajili ya kujenga amani na mshikamano wa Taifa kwa mwaka 2023

Na Mussa Mtepa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 kitaifa zitakazofanyika tarehe 1 Aprili 2023 Mkoani Mtwara.

Mazingira na Utunzaji wa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa

Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo 30 Machi 2023 katika viwanja vya Nangwanda Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amesema kuwa baada ya uzinduzi, Mwenge huo utakimbizwa katika mikoa 31, Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja na viongozi wengine wakitoa taarifa za maandalizi ya mwenge wa Uhuru. Picha na Mussa Mtepa

Amesema kuwa kipindi chote cha kuukimbiza Mwenge wa Uhuru utafanya kazi ya kuhamasisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuwahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao.

Waziri amesema ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu unazingatia umuhimu wa kuhifadhi Mazingira na Utunzaji wa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amesema mkoa umejipanga kuhakikisha uzinduzi huo unafanyika kikamilifu huku Ulinzi na Usalama ukiwa wa Kutosha huku akiwakaribisha wageni na wananchi kuhudhuria uzinduzi huo.