Jamii FM
Jamii FM
1 May 2026, 15:39

TASA yazindua mradi Mtwara kuwajengea uwezo wanawake na vijana katika utunzaji wa mazingira na usawa wa kijinsia, ikitumia sanaa kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu na kuacha vitendo vinavyoharibu mazingira
Na Musa Mtepa
Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Safaty Alliance (TASA), lenye makao makuu yake mjini Mtwara, Aprili 30, 2026 limefanya uzinduzi na utambulisho wa mradi katika ngazi ya jamii unaohusu wanawake na vijana katika ustahimilivu kwenye masuala ya mazingira na usawa wa kijinsia.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo uliofanyika katika Kijiji cha Nanguruwe, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Meneja Miradi wa shirika hilo, Betty Chenge, amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa miwili ya Mtwara na Ruvuma. Ameeleza kuwa sababu ya kuutekeleza katika maeneo hayo ni kutokana na shughuli zinazofanywa na wakazi, hususan kilimo cha kuhama hama na ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya mkaa.

Aidha, Betty Chenge amesema njia iliyotumika katika kutambulisha mradi huo ni sanaa ya maigizo pamoja na ngoma za asili zilizobeba ujumbe kuhusu namna wananchi wanavyoweza kutunza mazingira yao na kuepukana na vitendo kama ukataji wa miti hovyo, pamoja na maandalizi ya mashamba kwa njia ya kuchoma au kilimo holela.
Naye Jackline Mpunjo kutoka shirika rafiki la SDA amepongeza hatua ya TASA kwa kutumia njia sahihi ya ushirikishwaji wa wananchi kupitia maigizo na mdahalo. Amesema mbinu hiyo imewawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika kutoa suluhu za namna ya kutunza mazingira, ikiwa ni pamoja na kuhamasishana kupanda miti na kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji na Kata ya Nanguruwe wameonesha kufurahishwa na elimu waliyoipata katika uzinduzi huo, huku wakiahidi kuifanyia kazi katika maisha yao ya kila siku, hasa katika masuala ya usawa wa kijinsia na utunzaji wa mazingira.
