Jamii FM
Jamii FM
14 August 2026, 11:52

Ummy Mohamedi Fadhili, mkazi wa Ding’wida, Mtwara, amelalamikia kunyimwa nyumba aliyodai ilinunuliwa kwa fedha alizopata baada ya kuuza nyumba yake ya Tandahimba, akisema mzazi mwenzake anadai ni mali ya mtoto wao
Na Mwanahamisi Chikambu
Mwanamke mmoja, Ummy Mohamedi Fadhili, mkazi wa Kijiji cha Ding’wida, Kata ya Moma, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, amelalamikia kunyimwa haki ya kumiliki nyumba aliyodai kuinunua kwa fedha zilizopatikana baada ya kuuza nyumba nyingine aliyokuwa akiimiliki wilayani Tandahimba.
Akizungumza na Jamii FM, Ummy, ambaye amesema anasumbuliwa na magonjwa mbalimbali, ameeleza kuwa baada ya kutengana na mzazi mwenzake, alihamia wilayani Tandahimba ambako alianzisha makazi na baadaye kununua nyumba.
Ummy amesema kutokana na changamoto za kiafya alilazimika kuiuza nyumba hiyo, na fedha alizopata alimkabidhi mtoto wake ili amnunulie nyumba nyingine, akilenga kupata sehemu ya kuishi na kujiuguza akiwa nyumbani.
Hata hivyo, amesema alipofika katika nyumba hiyo alikumbana na hali tofauti baada ya mzazi mwenzake kumweleza kuwa nyumba hiyo si mali yake bali ni ya mtoto wao.
Ummy amesema alifikisha malalamiko yake kwa viongozi wa kijiji ambao waliwaita yeye na mzazi mwenzake kwa ajili ya kusikiliza pande zote, ambapo walimshauri mzazi mwenzake kutotumia mali hiyo bila makubaliano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sogea, Kijiji cha Ding’wida, Kata ya Moma, Musa Mitumba, amesema ofisi yake imepokea taarifa kuhusu mgogoro huo na imekuwa ikitoa ushauri kwa pande zote kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo.