Jamii FM

Wananchi wa Masugulu waishukuru serikali mradi wa maji

14 August 2026, 08:39

Mwonekano wa juu wa eneo la kuchujia maji la mradi wa maji mto Ruvuma katika kijiji cha Masugulu wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara(Picha na Mtwara Rs)

Wananchi wa Masugulu wameishukuru serikali kwa mradi wa maji wa Mto Ruvuma wenye thamani ya Sh bilioni 43.2, uliotekelezwa kwa asilimia 96, wakiamini utaondoa tatizo la maji na hatari ya mashambulizi ya mamba

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Kijiji na Kata ya Masugulu, wilayani Nanyumbu, wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma, wakisema utamaliza kwa kiasi kikubwa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa Masugulu, Wilaya ya Nanyumbu na baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Masasi.

Wakizungumza August 10, 2026 wakati wa ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, ambaye pia ni mlezi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Mtwara, wananchi hao wamesema tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho hawajawahi kupata huduma ya maji safi na salama, bali wamekuwa wakitegemea maji ya Mto Ruvuma.

Aidha, wameeleza kuwa kwa miaka mingi baadhi ya wakazi wamepoteza viungo na hata maisha baada ya kushambuliwa na mamba walipokuwa wakifuata maji mtoni, hivyo wanaamini mradi huo utaondoa hatari hiyo na kuboresha maisha ya wananchi.

Sauti ya 1 wananchi wa Masugulu
Picha ya juu ikionesha eneo na chanzo cha maji cha Mto Ruvuma kilicho chimbwa katika Mto Ruvuma katika kijiji cha Masugulu jirani na Mtambaa swala(Picha na Mtwara Rs Habari)

Kwa upande wake, Mhandisi Elekezi wa Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma unaotekelezwa na MANAWASA kwa ajili ya kuhudumia Mangaka, Masasi na maeneo jirani, amesema mradi huo unagharimu shilingi bilioni 43.2, ambapo hadi sasa shilingi bilioni 35.627 zimetumika na utekelezaji umefikia asilimia 96.

Sauti ya 2 Mhandisi Elekezi wa Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma

Akizungumza kwa niaba ya Serikali kama Waziri mlezi wa miradi ya maendeleo mkoani Mtwara, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amewataka wananchi wa Masugulu na vijiji jirani kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji ili kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kuwa endelevu na yenye manufaa kwa jamii.

Sauti ya 3 Judith Kapinga Waziri wa Viwanda na Biashara

Mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma unaotekelezwa wilayani Nanyumbu ni miongoni mwa miradi 28 ya usambazaji wa maji mijini inayotekelezwa nchini, ukiwa na lengo la kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.