Jamii FM

Wananchi Newala waishukuru serikali kwa umeme

23 July 2026, 12:54

Baadhi ya Wananchi wa wilaya ya Newala wakifuatilia kwa ukaribu hotuba ya Waziri wa Nishati Deogratious Ndejembi July 21,2026 alipozingua laini ya umeme yenye msongo wa kilovoti 33. Picha na Musa Mtepa

Wananchi wa Newala wameishukuru Serikali kwa kuzindua laini ya umeme wa kV 33 kutoka Masasi hadi Newala, wakisema itaimarisha shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji wa wajasiriamali na kuboresha huduma zinazotegemea umeme wa uhakika

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Wilaya ya Newala mkoani Mtwara wameishukuru Serikali kwa kuwapatia laini ya umeme wa msongo wa kilovoti 33, wakisema hatua hiyo itachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Wakizungumza mara baada ya uzinduzi wa laini hiyo uliofanyika Julai 21, 2026, wananchi hao wamesema umeme wa uhakika utawasaidia wajasiriamali wadogo kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, tofauti na ilivyokuwa awali walipokuwa wakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme.

Mjasiriamali wa Newala, Mwajuma Rashidi, amesema umeme huo utamwezesha kuimarisha shughuli zake za uzalishaji wa bidhaa kama ice cream, juisi na huduma nyingine zinazohitaji umeme wa uhakika.

Sauti ya Mwajuma Rashidi – Mjasiriamali, Newala

Aidha, Mwajuma amesema ukosefu wa umeme wa uhakika uliwahi kusababisha baadhi ya wafanyabiashara wa samaki wabichi kusitisha biashara zao kutokana na kushindwa kuhifadhi bidhaa hizo. Ameeleza kuwa ujio wa laini mpya ya umeme utawapa fursa ya kurejea na kuendeleza biashara zao.

Sauti ya Mwajuma Rashidi – Mjasiriamali, Newala

Kwa upande wake, Bi. Maimuna Mshamu, pamoja na wananchi wengine, wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, huku wakiiomba kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika unaimarishwa zaidi kupitia mpango wa kuiunganisha mikoa ya kusini kwenye Gridi ya Taifa.

Sauti ya Maimuna Mshamu – Mkazi wa Newala

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa laini ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 76 kutoka Masasi hadi Newala, Waziri wa Nishati, Deogratious Ndejembi, amesema uzinduzi huo si mwisho wa safari bali ni mwanzo wa utekelezaji wa mpango mkubwa wa Serikali wa kuiunganisha mikoa ya Mtwara na Lindi kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme ili kuongeza uhakika wa huduma hiyo na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Sauti ya Deogratious Ndejembi – Waziri wa Nishati