Jamii FM

Maeneo yanayochipua mapema Mikorosho yapewa kipaumbele Pembejeo

25 May 2026, 10:42

Mwonekano wa Mkorosho ambao tayari umechipua ukiwa tayari kwa ajili ya viuatilifu ikiwa hatua ya uzalishaji wa zao la Korosho (Picha na Musa Mtepa)

Bodi ya Korosho Tanzania imesema usambazaji wa pembejeo za ruzuku kwa msimu wa 2026/2027 umeanza katika maeneo yanayowahi kuchipua mikorosho, huku wakulima wakitakiwa kutumia utaratibu ule ule wa usajili kupitia AMCOS

Na Musa Mtepa

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imesema usambazaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali umeanza katika maeneo yanayowahi kuchipua mikorosho kuliko maeneo mengine yote yanayozalisha korosho nchini.

Hayo yameelezwa Mei 22, 2026 na Meneja wa Mipango ya Kilimo wa CBT, Juma Yusuf, katika mahojiano maalumu kwenye kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Redio mjini Mtwara kuhusu ugawaji wa pembejeo za ruzuku kwa msimu wa 2026/2027.

Amesema pamoja na uzinduzi wa mapema wa usambazaji wa viuatilifu unaofanywa na KCJE msimu huu, maeneo yaliyopewa kipaumbele ni yale yanayowahi kuchipua mikorosho, ikiwemo baadhi ya kata za wilaya za Kilwa, Tandahimba, Halmashauri ya Mtama pamoja na baadhi ya maeneo ya Mtwara.

Sauti ya 1 – Juma Yusuf, Meneja wa Mipango ya Kilimo CBT

Aidha, Juma Yusuf amesema CBT imejipanga kushirikiana kwa karibu na sekretarieti za mikoa, halmashauri za wilaya pamoja na serikali za mitaa ili kuhakikisha changamoto zozote zinazoweza kusababisha ucheleweshaji wa pembejeo kwa wakulima katika msimu wa 2026/2027 zinatatuliwa kwa wakati.

Sauti ya 2 – Juma Yusuf, Meneja wa Mipango ya Kilimo CBT

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA wa Bodi ya Korosho Tanzania, Gerard Rogati, amesema utaratibu wa wakulima kupata pembejeo za ruzuku kwa msimu wa 2026/2027 utaendelea kuwa ule ule uliotumika msimu uliopita. Amesema mkulima aliyesajiliwa anatakiwa kwenda kwenye Chama cha msingi cha ushirika (AMCOS) akiwa na namba yake ya simu aliyotumia wakati wa usajili.

Sauti ya Gerard Rogati – Afisa TEHAMA CBT

Akijibu swali la msikilizaji aliyependa kufahamu kuhusu mkulima aliyenunua shamba kutoka kwa mkulima aliyekuwa amesajiliwa awali kwa ajili ya kupata pembejeo za ruzuku, Gerard Rogati amesema mmiliki mpya atalazimika kuwasilisha nyaraka husika kwenye mfumo ili aweze kuthibitishwa na kupata pembejeo hizo.

Sauti ya Gerard Rogati – Afisa TEHAMA CBT