Jamii FM
Jamii FM
1 July 2026, 06:36

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Maryprisca Mahundi, amezindua Mfuko wa Uwezeshaji wa Wanawake Wajasiriamali Wadogo Mtwara Mjini, ambapo wanawake zaidi ya 300 wamepatiwa mafunzo na 80 kunufaika na mikopo ya biashara.
Na Musa Mtepa
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Maryprisca Mahundi, leo Juni 30, 2026 amezindua rasmi Mfuko wa Uwezeshaji wa Wanawake Wajasiriamali Wadogo katika jimbo la Mtwara mjini mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mahundi amesema wanawake wengi ndio wanaobeba jukumu la kulea familia, kusomesha watoto, kutunza afya za kaya pamoja na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali, hivyo ni muhimu kuendelea kuwawezesha kiuchumi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Hata hivyo, Naibu Waziri amewataka wanawake kulinda ndoa zao na kutumia fursa za kiuchumi kwa manufaa ya familia na jamii, badala ya kutumia mafanikio ya kiuchumi kwa njia zinazoweza kusababisha migogoro ya kifamilia.

Aidha, Mahundi amempongeza Dkt Joel Nanauka kwa kuwajengea wanawake uwezo wa kutambua thamani ya fedha, kukopa kwa malengo pamoja na kuwapatia elimu ya ujasiriamali.
Amesema kupitia mpango huo, zaidi ya wanawake wajasiriamali 300 wamejengewa uwezo huku wanawake 80 wakipatiwa mikopo kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Dkt Joel Nanauka, amesema kupitia Programu ya Uwezo, lengo ni kujenga msingi wa uchumi jumuishi unaompa kila mwanamke wa jimbo hilo fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya familia yake na jamii kwa ujumla.
Aidha, Dkt Nanauka amesema Mfuko wa Uwezeshaji wa Wanawake Wajasiriamali Wadogo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupimwa kwa miundombinu pekee, bali pia kwa uwezo wa wananchi kujipatia kipato, kuendesha biashara zenye tija na kuboresha maisha ya familia zao.

Wakizungumzia uzinduzi wa mfuko huo kupitia Nanauka Foundation, baadhi ya wanawake wajasiriamali wadogo wamemshukuru Dkt Nanauka kwa kutimiza ahadi yake ya kuwawezesha kiuchumi.
Wanawake hao wameahidi kutumia vyema elimu na mikopo waliyoipata ili kuendeleza biashara zao, kuboresha kipato cha familia zao na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.
