Jamii FM

TPB yatoa elimu kwa wavuvi

23 April 2021, 19:31 pm

Na Karim Faida

Wavuvi wa kijiji cha Namela kata ya Msangamkuu halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani hapa wamepewa elimu ya namna ya kupata mkopo Benki ili kujiendeleza katika shughuli zao kwa lengo la kuvua kivuvi chenye tija.
Kaimu Meneja wa Benki ya Posta tawi la Mtwara Ndugu Maina Mbawala akizungumza na wavuvi

Akiongea na wavuvi hao leo katika viunga vya jengo la Msalaba mwekundu kata ya Shangani mkoani hapa, Kaimu Meneja wa Benki ya Posta tawi la Mtwara Ndugu Maina Mbawala amefurahishwa kwa kitendo cha Taasisi ya Beach Management Unit BMU inayojihusisha na uhifadhi wa rasilimali za bahari kutoka kijiji cha Namela kuwakutanisha wavuvi na Meneja huyo kwa lengo la kujifinza mambo mbalimbali ikiwa na pamoja na kujua vigezo vya kupata mkopo kutoka kwenye Benki hiyo. Katika maelezo yake Kaimu Meneja huyo amesema yupo tayari kuwapa mikopo wavuvi hao.

Diana Shuma ambae ni Afisa mawasiliano kutoka shirika la WWF

Nae Diana Shuma ambae ni Afisa mawasiliano kutoka shirika la WWF linalojihusisha na uhifadhi wa mazingira ya bahari na ambalo ndio mfadhili wa Taasisi ya BMU, amesema jambo lililofanywa na Taasisi hiyo ni kubwa kwa kuwa itawasaidia wavuvi hao kuvua kwa tija maana watanunua vifaa vya kisasa vya uvuvi baada ya kutimiza vigezo vya Benki na kupata mkopo.

Wananchi walifuatilia maelekezo

Bi Diana amesema WWF wamekuwa wakifanya kazi na Taasisi ya BMU tangu mwaka 2018 na wamewasaidia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwajengea ofisi, kuwanunulia boti ambayo inasaidia kufanya doria ili kuendelea kulinda bahari, wamejenga soko la katika eneo la Ndokwa, wametoa mafunzo ya uhifadhi ya bahari n.kKwa upande wake Katibu wa mipango na fedha kutoka kwenye Taasisi hiyo Ndugu Mahafudhi Ally amesema lengo la kuwakutanisha Wavuvi na Taasisi hiyo ya fedha ni kuwasaidia wavuvi wao kupata mikopo itakayowasaidia kununua baadhi ya vifaa muhimu na hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na hata vikundi.

Akiongea na Jamii fm radio, Ndugu Mohamedi Namcholo ambae ni mvuvi kutoka kijiji cha Namela ameishukuru Taasisi ya BMU kwa kuwakutanisha na Benki ya Posta na ameahidi kulipa mkopo huo kwa haraka endapo watafanikiwa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Namela Ndugu Juma Mzee amewataka wavuvi kuendelea kushirikiana na Taasisi hiyo ya BMU ili kuendeleza utunzaji wa rasilimali za bahari. Pia amewataka wavuvi kuitumia vizuri mikopo yao ili kutimiza malengo ya mikopo hiyo.

Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi wa wavuvi kutoka kwenye vikundi tisa, Vinane vikitokea Kijiji cha Namela na kimoja kutoka Kijiji cha Sinde.