Jamii FM

TAMCU yauza ufuta mnada wa kwanza bei ya juu shilingi 2520

22 May 2026, 14:00

Baadhi ya wakulima wa zao la ufuta wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakifutilia mnada wa wa zao hilo

TAMCU yauza zaidi ya tani 994 za ufuta katika mnada wa kwanza Tunduru kwa wastani wa shilingi 2,477 kwa kilo, huku viongozi wakisisitiza malipo ya wakulima kufanyika kwa wakati

Na Musa Mtepa

Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao na Masoko cha TAMCU kilichopo wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, kimeuza zaidi ya tani 994.6 za ufuta katika mnada wa kwanza wa msimu wa mwaka 2026/2027.

Mnada huo umefanyika Mei 21, 2026 katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru kupitia mfumo wa Soko la Biashara ya Mazao na Bidhaa kwa njia ya mtandao (TMX).

Akizungumzia matokeo ya mnada huo, Mwenyekiti wa TAMCU, Bw. Musa Manjaule, amesema jumla ya kilo 994,618 za ufuta ziliingizwa sokoni, huku wanunuzi sita wakishiriki katika mnada huo.

Aidha, Bw. Manjaule amesema wamefanikiwa kuuza ufuta kwa bei ya juu ya shilingi 2,520 kwa kilo, bei ya chini ikiwa shilingi 2,410, na wastani wa bei ukiwa shilingi 2,477 kwa kilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Denis Masanja, ameipongeza TMX kwa kuendesha mnada huo kwa mfumo wa kisasa na wa uwazi, akieleza kuwa kila hatua ya mnada ilikuwa wazi kwa washiriki wote.

Aidha, Mheshimiwa Masanja amewataka viongozi wa TAMCU kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao za mauzo ya mnada wa kwanza kwa wakati.

Nao baadhi ya wakulima waliohudhuria mnada huo wamekubali kuuza ufuta wao kwa bei zilizopatikana, huku wakiomba bei kuongezeka katika minada ijayo.

Sauti ya wakulima wa ufuta Tunduru
Ufuta ukiwa umehifadhiwa Ghalani tayari kwa kuuza (Picha kwa msaada wa mtandao)