Jamii FM
Jamii FM
1 July 2026, 11:11

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewataka wazazi na walezi kushirikiana kutokomeza ukatili dhidi ya watoto huku akibainisha kuwa zaidi ya matukio 710 yaliripotiwa mkoani humo kati ya Julai 2025 na Machi 2026.
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewataka wazazi na walezi kushirikiana kwa karibu katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kujitokeza katika Jamii.
Akizungumza Juni 30, 2026, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika mkoani Mtwara, Kanali Msengi amesema kuwa ni wajibu wa kila mwanajamii kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya aina zote za ukatili unaofanyika dhidi yao.
Aidha, Kanali Msengi amesema kuwa licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto, bado mkoa unakabiliwa na changamoto za ukatili majumbani na mashuleni, mimba za utotoni pamoja na tatizo la utoro shuleni.
Amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, zaidi ya matukio 710 ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa katika Mkoa wa Mtwara.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amewahimiza watoto kutoa taarifa wanapofanyiwa vitendo vya ukatili kwa kuwaeleza watu wazima wanaowaamini au vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kuhusu matukio hayo 710 ya ukatili, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mtwara, Bi Tabitha Kilangi, amesema kuwa kesi hizo zimeendelea kushughulikiwa katika ngazi mbalimbali.
Amesema kuwa kesi 400 zimetatuliwa kupitia madawati ya ustawi wa jamii, kesi 250 zimefikishwa polisi na zinaendelea na uchunguzi, huku kesi 50 zikiwa mahakamani zikisubiri maamuzi.

Hata hivyo, Bi Kilangi amesema bado kuna haja ya kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu malezi chanya, ili kusaidia watoto kukua katika mazingira yenye maadili mema na hatimaye kuwa watu wazima wenye maadili na mchango chanya kwa jamii.