Jamii FM
Jamii FM
13 July 2026, 17:26

Wanachama wa MFICO’S Msangamkuu wameiomba serikali kukamilisha vifaa vya boti ya mkopo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 102, wakisema upungufu wa vifaa umewazuia kuanza uvuvi na kurejesha mkopo
Na Musa Mtepa
Wanachama wa Chama cha ushirika cha msingi cha wavuvi (MFICO’S) katika kata ya Msangamkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali kuwakamilishia vifaa vilivyobaki vya boti ya mkopo waliyopewa zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wanachama hao wamesema tangu walipopokea boti hiyo yenye thamani ya Sh milioni 102,285,112.43 Machi 6, 2024, hawajaanza kuitumia kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya vifaa muhimu, hali inayowazuia kuanza shughuli za uvuvi na hivyo kushindwa kuanza kurejesha mkopo huo.
Aidha, wamesema baada ya kubaini kuwa baadhi ya vifaa vilivyotakiwa havipo, waliandika barua kwenda Wizara husika kueleza changamoto hiyo, lakini hadi sasa hawajapata majibu rasmi.
Akifafanua changamoto hiyo, Katibu wa kujitolea wa Chama cha ushirika cha wavuvi MFICO’S, kata ya Msangamkuu, Maabadi Ibrahim Salumu, amesema mkopo huo ulihusisha boti ya uvuvi (fiberglass) yenye urefu wa mita 12, injini ya boti, nyavu 11, maboya 600, kamba, kifaa cha kutambua maeneo ya samaki (fish finder) pamoja na pampu ya kutoa maji ndani ya chombo. Hata hivyo, baada ya kupokea vifaa hivyo walibaini kuwa baadhi ya vifaa muhimu kwa aina ya uvuvi waliokusudia havikuwemo.
Katibu amesema baada ya kufanya tathmini waligundua kuwa vifaa vilivyokosekana vina thamani ya takribani Sh milioni 16, kiasi ambacho amesema ni kigumu kwa chama kukipata kwa wakati.

Ameongeza kuwa kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kuanza kutumia boti hiyo huku muda wa kuanza marejesho ya mkopo ukikaribia, wanaiomba Serikali kuwasaidia kupata vifaa vilivyobaki ili waanze shughuli za uvuvi.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Kusini, Wilson Magodi, amesema jukumu la TADB katika mradi huo ni kusimamia marejesho ya mkopo. Amesema kutokana na changamoto zinazowakabili MFICO’S, wameendelea kuwashauri kutafuta njia mbadala za kupata fedha za kukamilisha vifaa vinavyokosekana ili waanze shughuli za uvuvi na marejesho ya mkopo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo, Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni msimamizi wa mradi huo, Clemence Katunzi, amesema changamoto za upungufu wa vifaa zilihusu boti zenye urefu wa mita saba na si boti ya mita 12 kama wanavyodai wanachama wa MFICO’S.
Ameeleza kuwa mkataba wa mkopo wa boti ya mita 12 haukujumuisha vifaa kama jenereta na taa, hivyo haviwezi kuhesabiwa kuwa ni sehemu ya vifaa vilivyopaswa kutolewa chini ya mkataba huo.
Hata hivyo, Katunzi amesema ndani ya mwezi huu Serikali inatarajia kutoa vifaa vya ziada ikiwemo kamba na madingi, ambavyo havikuwemo kwenye mkataba wa awali wa mkopo.
Katunzi pia amewataka wavuvi kuhakikisha wanatumia kikamilifu fursa wanazopewa na Serikali ili miradi hiyo iweze kuwanufaisha wao pamoja na kutoa nafasi kwa vikundi vingine kupata msaada wa aina hiyo.
Aidha, amethibitisha kuwa Wizara ilipokea barua za MFICO’S na kwamba badala ya kujibu kwa maandishi, maafisa wa Wizara walifika katika eneo husika, wakazungumza na wanachama hao na kufanya tathmini ya changamoto zilizokuwapo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
