Jamii FM

Kijiji chakusanya Tsh. 150,000 Septemba 2025-Aprili 2026

28 April 2026, 18:48

Wananchi wa kijiji cha Kitaya wakiwa katika mkutano (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa Kitaya wajadili mapato, matumizi na changamoto za uongozi, wakitaka uwazi zaidi huku viongozi wakiiomba serikali kutatua sintofahamu inayokwamisha maendeleo ya kijiji

Na Musa Mtepa

Kijiji cha Kitaya, Aprili 24, 2026 kimefanya mkutano mkuu wa kijiji wenye lengo la kupitia taarifa mbalimbali za maendeleo pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho.

Akisoma taarifa ya mapato na matumizi kwa kipindi cha Septemba 1, 2025 hadi Aprili 20, 2026, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Kitaya, ambaye pia ni Mtendaji wa Kijiji cha Dindwa, Mustafa Mlango, amesema kuwa katika kipindi hicho kijiji kimekusanya shilingi 150,000/= huku matumizi yakifikia shilingi 140,000/=, na kuacha salio la shilingi 10,000/= pekee.

Sauti: Mustafa Mlango – Kaimu Mtendaji, Kijiji cha Kitaya

Wakichangia ajenda hiyo, baadhi ya wananchi wametaka ufafanuzi wa taarifa za ukusanyaji wa mapato kwa vipindi vya nyuma, hususan mapato yatokanayo na maegesho ya magari pamoja na mapato ya ghala la kijiji katika msimu wa korosho wa mwaka 2025/2026.

Sauti: Wananchi wa Kijiji cha Kitaya

Aidha, wananchi hao wameeleza kuwa sintofahamu iliyopo katika ukusanyaji wa mapato inachangiwa na ukosefu wa uongozi unaotambulika rasmi, hali inayodaiwa kusababishwa na kutokuaapishwa kwa wajumbe wa serikali ya kijiji waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.

Sauti: Wananchi wa Kijiji cha Kitaya

Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto za ukusanyaji wa mapato pamoja na uongozi wa kijiji, Abilahi Dadi Limila, ambaye ni mwenyekiti ambaye hatambuliwi na baadhi ya wananchi, ameeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na mvutano wa kisiasa unaoathiri utekelezaji wa majukumu ya uongozi.

Sauti: Abilahi Dadi Limila – Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitaya

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kitaya, Mhe. Abdala Chalamanda, ameiiomba serikali kusaidia kutatua sintofahamu hiyo ili kuwezesha ukusanyaji mzuri wa mapato na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika kijiji hicho.

Sauti: Abdala Chalamanda – Diwani wa Kata ya Kitaya