Jamii FM
Jamii FM
15 May 2026, 09:04

Madiwani wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wameeleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa TACTICS, huku viongozi wakitaka usimamizi madhubuti ili mradi huo uweze kuwanufaisha wananchi
Na Musa Mtepa
Baraza la madiwani la Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara limeeleza kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi anayetekeleza mradi wa TACTICS.
Hayo yamesemwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Mei 14, 2026, katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) tawi la Mtwara, hali inayozua maswali kwa madiwani pamoja na wanufaika wa mradi huo ambao ni wananchi wa Mtwara Mikindani.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Hassan Nyange, amekiri kuwepo kwa kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia tano pekee, tofauti na matakwa ya mkataba.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mheshimiwa Said Zaidi, amemtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuhakikisha anaufuatilia kwa karibu mradi wa TACTICS ili uweze kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Mtwara Mikindani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mheshimiwa Abdallah Mwaipaya, amewataka madiwani kuhakikisha wanatatua kero za wananchi pamoja na kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mradi wa TACTICS katika Manispaa ya Mtwara Mikindani unahusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara za lami za Chuno zenye urefu wa takriban kilomita 3.38 na Samia City Access Road yenye urefu wa takriban kilomita 2.4. Aidha, mradi huo unajumuisha ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua eneo la Kiyangu kwa ajili ya kupunguza mafuriko, ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi Chipuputa, kituo cha wajasiriamali na viwanda vidogo eneo la Skoya pamoja na majengo ya usimamizi wa miradi na huduma nyingine za kijamii.
Mradi huo una thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 27 kwa Manispaa ya Mtwara Mikindani pekee, ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi mwaka 2025 chini ya mkandarasi M/S Serengeti Limited