Jamii FM
Jamii FM
18 July 2026, 10:55

TARI Naliendele imetoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu kuhusu kilimo bora cha korosho, ikiwajengea uwezo wa kutumia mbegu bora na kudhibiti magonjwa ili kuongeza uzalishaji na tija
Na Musa Mtepa
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Naliendele mkoani Mtwara, leo Julai 17, 2026, imeendesha mafunzo maalumu kwa watu wenye ulemavu yaliyolenga kuwajengea uwezo kuhusu kilimo bora cha zao la korosho.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa TARI Naliendele ambaye pia ni Mtafiti Mkuu, Dkt. William Mbasa, amesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha makundi yenye mahitaji maalumu yanapata elimu ya kilimo bora ili kuongeza uzalishaji na kuinua kipato.
Amesema mafunzo hayo yamejikita katika matumizi ya mbegu bora, miche iliyoboreshwa ya korosho, pamoja na mbinu sahihi za kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa mikorosho.

Kwa upande wake, Mtafiti wa TARI Naliendele, Dkt. Salumu Mapua, ambaye aliendesha mafunzo hayo, amesema lengo ni kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu ili washiriki kikamilifu katika uzalishaji wa korosho wenye tija na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya taifa ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Ameongeza kuwa washiriki wamepatiwa elimu ya kutambua magonjwa na wadudu waharibifu wa mikorosho pamoja na njia bora za kudhibiti changamoto hizo.

Naye Duasi Gambo, mtafiti kutoka TARI Naliendele, amesema mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kutumia mbegu na miche bora ya korosho, hatua itakayosaidia kuongeza mavuno na tija katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Mtwara, Mohamedi Omari (Mr. Langa), amesema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa watu wenye ulemavu, hasa wale wanaojishughulisha na kilimo.
Ametoa wito kwa watu wengine wenye ulemavu kujikita katika shughuli za kilimo ili kujiongezea kipato na kupunguza utegemezi katika maisha yao ya kila siku.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TARI Naliendele kwa kuwapatia elimu hiyo, wakisema itawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo na kuongeza uzalishaji. Pia wameahidi kuendelea kutembelea kituo hicho ili kupata elimu zaidi kuhusu teknolojia na mbinu bora za uzalishaji wa mazao.

Mafunzo hayo ya siku moja yamewakutanisha watu wenye ulemavu mbalimbali, wakiwemo wasioona, wasiosikia na wenye ulemavu wa viungo, yakilenga kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu bora za kilimo cha korosho pamoja na kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa zao hilo.
