Jamii FM
Jamii FM
8 July 2026, 13:15

UTPC imeanza mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari wanawake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia mtandaoni, kuimarisha usalama wa kidijitali na kupata msaada wa kisheria wanapokumbana na vitisho.
Na Grace Hamisi
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umeanza rasmi mafunzo ya siku nne kwa waandishi wa habari wanawake yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia mtandaoni.
Mafunzo hayo yameanza Julai 6 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 9, 2026, katika Hoteli ya Nashera mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yanawakutanisha waandishi wa habari wanawake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, yakilenga kuwapatia maarifa na mbinu za kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, kuimarisha usalama wao wa kidijitali, na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya uandishi kwa uhuru, usalama na ufanisi.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Kenneth Simbaya, amesema kuwa unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni ni changamoto kubwa inayowaathiri waandishi wengi wa habari, hususan wanawake. Amesema vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara ya kisaikolojia, kuhatarisha usalama wao na kuathiri utendaji wao wa kazi.

Naye Afisa wa UTPC, Edwin Kipungu, amewataka waandishi wa habari kutoa taarifa kwa Klabu zao za Waandishi wa Habari (Press Clubs) wanapokumbana na vitisho, unyanyasaji au madhara mengine yanayohusiana na kazi zao, ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria na usaidizi mwingine kwa wakati.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi unaotekelezwa na UTPC kwa kushirikiana na International Media Support (IMS), unaolenga kujenga mazingira salama ya kazi kwa waandishi wa habari wanawake na kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na changamoto za kidijitali.
