RC Mtwara: Wananchi jitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura
10 October 2024, 15:55 pm
Maeneo ya utawala kwa nchi nzima yalitangazwa na Waziri husika kutoka ofisi yar ais TAMISEMI September 16,2024 na baada ya kutangaza maeneo hayo wasimamizi wa uchaguzi kwa ngazi za halmashauri zote nchini zikiwemo na halmashauri (9) za mkoa wa Mtwara nazo zilitangaza.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa mkoani Mtwara wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Wito huo umetolewa na mkuu wa mkoa, Kanali Patrick Sawala, katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake.
Zoezi la kuandikisha wapiga kura litaanza rasmi kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024. Kanali Sawala amesisitiza umuhimu wa wananchi wenye sifa kujitokeza ili kuhakikisha wanapata haki yao ya kupiga kura.
Aidha, amewataka wanamtwara kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla, na amekumbusha sifa zinazohitajika kwa wapiga kura na wagombea.
Kanali Sawala pia amesisitiza umuhimu wa amani katika mchakato wa uchaguzi, akihimiza wananchi kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Mratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa mkoa wa Mtwara, Edith Shayo, amesema kuwa zoezi la uandikishaji litatumia jumla ya kata 91, mitaa 188, vijiji 785, na vitongoji 3421. Vituo vya upigaji kura vitakuwa 3627, vilivyopo katika kila halmashauri za mkoa.
Uchaguzi huu wa serikali za mitaa ni sehemu ya mchakato mkubwa wa kidemokrasia, na hatua za awali zimeshaanza kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu, viongozi wa dini, na vijana.