Jamii FM

TANESCO Mtwara wapewa siku 10 kukarabati mitambo ya kufua umeme

6 March 2021, 13:54 pm

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametoa agizo la kuhakikisha ndani ya siku 10 mashine mbili za kufua na kuzalisha umeme wa gesi asilia zinakamilika ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Mtwara na Lindi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwa kwenye mitambo ya kuzalisha umeme Mkoani Mtwara

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo jana Machi 5,2021 alipotembelea kituo cha kufua umeme wa gesi asilia kilichopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa ambapo kati ya mashine nne zilizoharibika mbili zimetengenezwa na zinafanya kazi katika uwezo wake wa juu na mbili bado mbovu.

Moja ya mtambo iliopo kwenye eneo la kuzalisha umeme

Mwaka jana mwezi Novemba Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alifanya ziara kituoni hapo na kubaini mashine nne hazifanyi kazi na ni mbovu, kwahiyo alituma timu ya kuja kufanya ukarabati na mashine mbili zimepona na mbili bado na kwa mujibu wa meneja wa kituo cha uzalishaji umeme Mkoani Mtwara Mhandisi Didasi Maleko amesema zingekamilika mwishoni mwa mwezi huu Machi,2021 jambo ambalo Waziri amekataa.

Waziri ametoa siku kumi kwa Meneja wa kituo cha uzalishaji umeme wa gesi asili Mhandisi Didasi Maleko na watendaji wote wa kituo hiko kuhakikisha ndani ya siku kumi ukarabati unakamilika na wasipokamilisha kwa wakati atakuja kuhamisha wafanyakazi wote wa kituo hiko na kuleta wengine ili kuimarisha ufanisi wa kazi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amefanya ziara ya siku moja mkoani Mtwara kwa kutembelea kituo cha kuzalisha umeme wa gesi asilia, kisima cha gesi kilichopo Kijiji cha Mtoriya Nanguruwe na amezindua huduma ya magari yanayotumia gesi asilia katika kiwanda cha saruji cha Dangote Mkoani hapa.

Credit: Gregory Millanzi