Jamii FM

Tamasha la michezo la Eastgate Day Care Center

2 July 2022, 20:06 pm

Wazazi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili kupunguza vitendo vinavyoashiria ukatili dhidi yao.

Hayo yamesemwa na Bi Ester Nyagari Mzazi wa Serafini Elman katika tamasha la michezo lililohusisha wanafunzi na wazazi yaliyoratibiwa na shule ya Watoto ya Eastgate iliyopo Shangani Mashariki Mjini Mtwara, akisisitiza kuwa wazazi hawana budi kuwa karibu na watoto kwani kuwa mbali kunaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya mtoto kwani kumekuwa na matukio wanayofanyiwa yenye sura ya ukatili hivyo kuwa karibu nao kutasaidia kupunguza vitendo hivyo.

 

Nae Bi Pendo Daudi Mtui Mzazi wa Daniela Dicksoni amesema kuwa wazazi wanatakiwa kuwa na ushirikiano kwa pamoja inapotokea tamasha kama hili michango itolewe kwani kumekuwa na uzito wakutoa kwani faida yake ni kubwa kwa watoto hao.

 

Kwa upande wake Meneja wa shule hiyo Bi Ummy Mpini amesema kuwa leo imekuwa siku ya furaha kwani imeweza kuwakutanisha wazazi na watoto na kucheza michezo kwa pamoja na kuona vipaji vya watoto wao.

 

Aidha Bi Mpini amewataka wazazi na walezi kuwa makini kukaa na watoto kuwa karibu nao kwani siku hizi kumekuwa na mambo mengi ya kikatili wanayofanyiwa watoto hivyo kuwa karibu na mtoto kutasaidia mtoto kueleza yale aliyofanyiwa kwa kuwa ameshatengenezwa kuwa pamoja na wewe.

 

Hili ni tamasha lililoratibiwa na uongozi wa shule ya watoto ya Eastgate kukiwepo michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa namba, kukimbia umbali wa mita 100 kwa watoto, kufukuza kuku kwa wazazi na walimu, zoezi la kupanga namba na kuimba lenye lengo la ushirikishwaji na kuwatanisha wazazi kwa pamoja na watoto katika michezo hiyo.