Jamii FM

Wanakijiji wahamasishwa kushiriki kwenye miradi

18 April 2021, 10:20 am

Na Karim Faida

Wananchi wa Kijiji cha Ngorongoro kata ya Nanguruwe Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani hapa wametakiwa kushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoletwa katika kijiji chao ili kuharakisha miradi hiyo.

Mwenyekiti wa kijiji Ndugu Saidi Ngulyungu akizungumza katika mkutano

Akiongea katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, Mwenyekiti wa kijiji hicho Ndugu Saidi Ngulyungu amesema pamoja na kuharakisha miradi hiyo pia hata pesa inayopatikana kama ushuru wa vitu mbalimbali kwenye kijiji hicho itatumika kwenye shuhhuli zingine hivyo kupunguza maswali hasa pale wananchi wanapotaka kujua Mapato na matumizi ya pesa ya kijiji.

“Tukiwa na umoja katika kujitolea kwenye miradi yetu itawapa nguvu wale wanaotuletea hiyo miradi kutuamini na kuendelea kutuletea miradi mingine bila kuwa na wasiwasi na sisi”

amesema Mwenyekiti huyo

Hayo yamekuja baada ya kusomwa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji kuanzia Oktoba hadi Disemba 2020 na Januari hadi Machi 2021 ambapo jumla ya shilingi 1,200,500 ilikusanywa kama mapato na Shilingi 721,100 ikitumika na kubaki 479,400.

Mzee Ally Nahama akiuliza kuhusu matumizi ya shilingi 70,000

Katika pesa iliyotumika, ilitajwa Shilingi 70,000 ambayo alilipwa fundi ujenzi aliyejenga shimo la choo cha shule ya msingi Ngorongoro ambapo Ndugu Ally Nahama mkazi wa kijijini hapo alihoji kuhusu pesa hiyo kwa kuwa mwanzo waliambiwa kila kitu ni bure.

Baadhi ya wananchi wakiwa katika mkutano huo

Hata hivyo mwenyekiti alitoa ufafanuzi na kusema kuna kazi za kitaalam ambazo sio za kujitolea ambazo ni lazima mtu alipwe isipokuwa kama kutakuwa na mjuzi wa hiyo kazi na akakubali kujitolea kufanya bure ni vizuri zaidi.