Jamii FM

Mnyachi mguu sawa kuwatumikia wananchi

12 December 2024, 10:27

Wanawake wapatao 78 katika kata ya Mkunwa wamefanikiwa kupata nafasi mbalimbali za uongozi huku Lukia Mnyachi akiwa Mwenyekiti wa Kijiji wa Kwanza na wa pekee katika historia ya kata ya Mkunwa.

Na Musa Mtepa

Mwenyekiti pekee wa Kijiji wa kike katika kata ya Mkunwa, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Lukia Mnyachi, amesema ataendelea kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, na kwamba atajitahidi kuwahudumia wananchi wa Kijiji cha Nyengedi kwa masuala muhimu.

Hayo ameyasema katika sherehe za kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa kiongozi wao, zilizofanyika Desemba 11, 2024 katika kijiji hicho.

Lukia amesema ataendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zinazowakabili, zikiwemo upatikanaji wa maji, masuala ya elimu, kuunda Baraza la Ushauri la Wazee, pamoja na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Sauti ya 1 Lukia Mnyachi Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi

 Aidha, ametumia fursa hiyo kufikisha baadhi ya changamoto kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa Mtwara Vijijini, Nashiri Pontiya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo.

Sauti ya 2 Lukia Mnyachi Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi

Katika sherehe hizo, Nashiri Pontiya amewahakikishia wananchi wa Nyengedi kuwa kero ya huduma ya maji itatatuliwa hivi karibuni

Sauti ya Nashir Pontiya Mwenyekiti wa CCM Mtwara vijijini
Mwenyekiti wa CCM Mtwara vijijini Nashiri Pontiya akizungumza na Wana CCM katika mkutano wa kuwashuru kuchaguliwa kwa Bi Lukia Mnyachi kuwa mwenyekiti wa Kijiji (Picha na Musa Mtepa)

Mwanahamisi Magimbi, mkazi wa Kijiji cha Nanyati, ameelezea furaha yake kuhusu kuchaguliwa kwa Lukia Mnyachi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi, akisema kuwa ni kiongozi wa kwanza na pekee wa kike katika vijiji vya kata ya Mkunwa, na kwamba hatua hiyo imeweka historia katika kata hiyo.

Sauti ya Mwanahamisi Magimbi mkazi wa Kijiji cha Nanyati Mtwara dc

Wanawake wapatao 78 katika kata ya Mkunwa wamefanikiwa kupata nafasi mbalimbali za uongozi, jambo linaloonyesha mabadiliko makubwa katika ushiriki wa wanawake katika masuala ya kijamii na kisiasa na ni ushahidi wa mafanikio ya wanawake katika kuchangia maendeleo ya jamii zao.

Hata hivyo, jambo la kipekee zaidi ni kuwa Lukia Mnyachi amekuwa mwenyekiti wa Kijiji wa Kwanza na wa pekee katika historia ya kata ya Mkunwa, hatua ambayo inaonyesha jinsi wanawake wanavyoendelea kuvunja vizingiti na kushika nafasi muhimu za uongozi.

Ufanisi huu ni alama ya mabadiliko ya kijinsia na una motisha kwa wanawake wengine kujiunga na uongozi, ili kuchangia kwa nguvu maendeleo endelevu katika jamii zao.