Jamii FM

Mtwara wamshangaa nahodha mwanamke

15 May 2021, 19:35 pm

Na Karim Faida

Wananchi mbalimbali wa Manispaa ya Mtwara mikindani wameonekana kumshangaa Nahodha anayeitwa Mayasa Mzandi ambaye ndiye amekuwa Nahodha wa kwanza katika kivuko cha Mv Mafanikio kinachofanya safari zake kutoka Feri Manispaa ya Mtwara Mikindani hadi Msangamkuu halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Nahodha Mayasa Mzandi, Nahodha wa kwanza katika kivuko cha Mv Mafanikio

Akiongea na Jamii fm radio katika kivuko hicho, Bi Mayasa amesema wakati anaanza kuendesha kivuko hicho mwaka 2015, watu wengi walimshangaa huku wakisema “Mmae Mmae” (Kimakonde) ikiwa na maana ya “Mwanamke, Mwanamke” lakini kwa sasa wamemzowea na amekuwa rafiki yao.

Kivuko Mv Mafanikio

Hata hivyo Bi Mayasa amesema kutokana na yeye kufanya kazi hiyo ambayo wengi wanaamini kuwa ni ngumu kufanya Mwanamke, atafungua safari mpya kwa mabinti ambao walikuwa na mtazamo wa kuwa Mwanamke hawezi kufanya kazi hiyo.

Pia ameongeza kuwa moja kati ya changamoto alizozipitia ni pamoja na kuzama na meli wakati yeye akiwa msaidizi wa Nahodha aliyekuwa akiendesha meli hiyo wakitokea visiwani Zanzibar kuja Tanzania bara na yeye alipona kwa kuwa alikuwa anajua kuogelea.